NAIROBI, Kenya
MWANARIADHA mwenye kasi zaidi barani Afrika Ferdinand Omanyala, ambaye ni raia wa Kenya, ameahidi kuvunja rekodi ya Usain Bolt rekodi ya mbio za mita 100.
Bolt aliweka rekodi hiyo mwaka 2009 alipomaliza mbio kwa sekunde 9.58 katika mashindano ya mbio za dunia. Omanyala naye alikaribia muda huo mwaka jana kwa kumaliza mbio kwa sekunde 9.77 katika mashindano ya Kip Keino Classic na kunyakua rekodi ya bara Afrika.
Muda huo ulimfanya kuwa nambari nane katika historia ya wanariadha wenye kasi zaidi; kwasasa Omanyala anajipanga kuivunja rekodi ya Bolt.
“Ninapopiga hatua katika taaluma yangu ya riadha, lengo lake kuu ni kuvunja rekodi ya dunia na nimekuwa nikisema hili. Watu hawaniamini, lakini nimaanini nitavunja rekodi ya dunia wakati mmoja,” alisema Omanyala.
Omanyala ambaye ni mwajiriwa wa Huduma ya Polisi amejipa muda wa miaka miwili kuivunja rekodi ya Bolt ambayo imedumu kwa miaka 13 sasa.
“Nina uhakika haitakuchua zaidi ya miaka miwili. Ninatazamia kukimbia kwa muda wa sekunde 9.6 msimu huu, kisha kuupunguza muda taratibu,” aliongeza Omanyala.
Omanyala alidai, Bolt ambaye kwa sasa amestaafu ni mmoja wa wanariadha ambao hawawezi kufikia viwango vyake kwa sasa. “Ninajisikia vizuri kwa sababu ina maana tunafanya kazi kwa bidii na kile tunachofanya mazoezi kinafanya kazi pia, kwa hivyo ninahisi furaha kuwa mtu mwenye kasi zaidi barani Afrika na tunaendelea kupanda ngazi.”