‘Mgombea tuliyenae anatosha 2025’

0

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulurhman Kinana amesema hakuna dhambi kwa kiongozi aliyeko madarakani anapomaliza Awamu ya Kwanza kupewa Awamu ya Pili aendelee kuongoza.

Kauli ya Kinana inatokana na ombi la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa kushauri Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ziridhie kutoa fomu moja ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na fomu hiyo ni ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, uliotumiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa Wilaya ya Ruangwa, Kinana alisema katika mkutano huo kila aliyesimama amezungumza mambo mazuri yanayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo ya wananchi.

Aliogeza kuwa, Rais Samia anaonesha njia kwa kupanga, kutafuta mikakati na kuweka vipaumbele na sasa Watanzania wanajivunia mafanikio na hata wana CCM wanaposema mgombea tuliyenaye anatosha kugombea mwaka 2025 nadhani kama wanasababu yoyote zaidi ya kutambua mchango wake mkubwa katika Taifa hili.

“Na Wana-CCM si dhambi kusema fomu ya mgombea urais ni moja kama wanaridhika na kiongozi aliyeko madarakani. Pia CCM tuna utaratibu wetu kiongozi akichukua Awamu ya Kwanza anapewa kuongoza na Awamu ya Pili.

“Rais Samia Suluhu Hassan yuko Awamu ya Kwanza, kwa nini asipewe Awamu ya Pili? Hakuna sababu ya kusema hapana. Kwa CCM kusema tumezingatia utaratibu wa chama chetu Rais anapomaliza kuongoza Awamu ya Kwanza anaingia ya Pili.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akielezea utekelezaji wa Ilani alisema: “Nisikosee mbele ya wajumbe wenzangu hawa kusema kwa vyovyote itakavyokuwa Ndugu Makamu Mwenyekiti tunaomba mkashauri kule Kamati Kuu na Halmashauri Kuu watoe fomu moja tu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 kama mgombea pekee wa CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here