Na Iddy Mkwama
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema, mfuko huo una afya tele na una uwezo wa kutoa huduma kwa miaka 30 ijayo.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263 marejeo ya mwaka 2015).
Lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara, wanaopatwa na changamoto ya kuumia, kuugua au kufariki wakiwa kwenye harakati za kutimiza majukumu yao ya kazi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Dkt. Mduma alisema, mfuko huo upo imara na unaendelea kupanua wigo wa huduma.
Alisema, kutokana na tathimini ya uhai wa uendelevu wa mfuko huo, iliyofanyika mara mbili, ikiwemo ile iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha mfuko huo una uwezo endelevu wa kulipa fidia mpaka mwaka wa fedha 2047/2048.
Mduma alisema, WCF ilifanya tathimini ya kwanza mwaka 2018 na nyingine mwaka 2022, na zote zimeonyesha mfuko huo ni himilivu na una uwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kutetereka kwa muda mrefu.
“Mfuko unaendelea kuimarika na unaendelea vizuri. Tupo imara kwa miaka 30 ijayo,” alisema Mduma na kuweka wazi mafanikio ambayo wanajivunia tangu mfuko huo ulipoanzishwa.
Akitaja baadhi ya mafanikio hayo Dkt. Mduma alisema, thamani ya mfuko huo imeongezeka, ambapo hadi kufikia Septemba, mwaka huu ilikuwa Shilingi Bilioni 697.5, hivyo mapato ambayo yanatokana na uwekezaji wa mfuko yameongezeka.
Alisema, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongezeka kwa wigo wa huduma, kupata hati safi “vile vile tumehakikisha tumejenga misingi mizuri ya kuufanya mfuko huu kuwa na uhai endelevu.”
Mbali na mafanikio hayo, Dkt. Mduma alisema, kwasasa mfuko huo unatoa mafao aina saba; Fao la ulemavu wa muda, ulemavu wa kudumu, ugonjwa, fao la utegemezi, fao la utengamao na fao la utegemezi.
“Fao la utengamao limelenga kumjengea uwezo mwajiriwa ambaye anapata ajali au ugonjwa kazini uwezo ili aweze kujitegemea licha ya changamoto ambayo amepitia akiwa kazini. Ulemavu wa muda, isi tunakulipa kwa kipindi ambacho wewe unaugua na hauwezi kumzalishia mwajiri wako,” alifafanua Dkt. Mduma.
Aidha, Mkurugenzi huyo alitaja vyanzo vya mapato ya mfuko huo kwasasa, ambapo ni michango ya waajiri na miradi yake ya uwekezaji ambayo ipo nchini.
“Uwekezaji wa mfuko hadi kufikia Septemba 2023 umeimarika na tumefanikiwa kulipa kodi ya Shilingi Bilioni 62.7. Hii ni kodi ya mapato ambayo inatokana na uwekezaji tu. Mwelekeo wa mfuko siku zijazo ni kupanua huduma zetu,” alisema Mkurugenzi huyo.
Pia, alisema wamejipanga kuimarisha huduma zao Kidigitali na kufungua huduma katika mikoa ya kimkakati nchini, ambapo hivi sasa huduma zao kwa asilimia 90% zinatolewa kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba amewaomba wanahabari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuhabarisha umma kuhusu mambo mbalimbali yanayofanyika nchini.