Na Iddy Mkwama, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema, kitafanya kampeni za kitaalam kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
Chama hicho kimesema, hakina shaka na ushindi wa kishindo wa mgombea wao Dkt. Hussein Mwinyi kutokana na mtaji alionao wa utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa makundi mbalimbali.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
Mbeto alisema, Dkt. Mwinyi kila mara amekuwa akitoa kauli kwamba hataki kuondoka na deni, ndio maana amejitahidi kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake, kutekeleza ahadi zake.
Alisema, Rais Mwinyi aliahidi kutengeneza mazingira mazuri ya masoko na mitaji jambo ambalo amelitekeleza, pia aliahidi kujenga barabara nzuri na ametekeleza na zinaonekana, naujenzi unaendelea.
“Aliahidi watoto Zanzibar watasoma kwenye mazingira mazuri, tunayaona. Aliahidi kuwapa matibabu bure tena ya kisasa mmeyaona,” alisema.
Mbeto akielezea zaidi ahadi alizotekeleza Rais Dkt. Mwinyi alisema, aliahidi kuwainua wazee kwenye huduma za kijamii ametekeleza, ambapo pamoja na mambo mengine, wazee wanalipwa posho kila mwezi.
“Tutapita kwenye makundi haya ili kuhakikisha na kuwaambia ambacho Rais Mwinyi ametekeleza kwao, anaenda kukutana na wanafunzi wa Vyuo Vikuu, aliwaahidi kila mtoto wa Kizanzibar atakayefaulu atapata mkopo, amelitekeleza hilo,”
Mbeto alisema, Dkt. Mwinyi kwenye suala la mikopo amefika mbali zaidi kwa kuishusha hadi kwa ngazi ya diploma, tofauti na awali walikuwa wanapewa wanafunzi wa digrii peke yao.
“Kwahiyo, anakwenda kukutana na makundi aliyoyapa ahadi na kutekeleza na wananchi wa Zanzibar wananufaika. Tumejiandaa vizuri, Mkutano wa uzinduzi wa kampeni utakuwa wa aina yake,” alisema Mbeto.