Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema moja ya msingi unaolijenga Taifa ni umoja, hivyo kila Mtanzania anapokuwa sehemu yoyote ana haki ya kupata huduma anayohitaji.
Chama hicho, kimetoa kauli hiyo kufuatia mjadala unaoendelea hivisasa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu wanalalamikia kubaguliwa kwenye huduma hususani za afya wakiwa Visiwani humu.
Akizungumza mjini hapa, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, viongozi wakuu Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuhakikisha Taifa linakuwa salama kwa kuhimiza umoja na mshikamano.
“Katiba ipo wazi, Taifa hili linaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na moja ya msingi unaolisimamia Taifa letu ni umoja, Mtanzania anapokuwa popote, ukiacha misingi tuliyoiweka ya Serikali, ana haki ya kupata huduma yoyote,” alisema Mbeto
Aliongeza, “huo ndio msingi wa Taifa, tunaizungumzia misingi ya kujenga Taifa letu, msikilize Rais Mwinyi anasemaje, msikilize Rais Samia, kutwa wanahimiza amani, wanazungumzia umoja na mshikamano Watanzania..”