Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji miradi ya kimkakati, ushawishi wake Kimataifa na kuaminika kwake sanjari na uamuzi wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika, kufanya mkutano wake Tanzania.
Kadhalika CCM kimeutaja uwezo wa Rais Dkt Samia Kimataifa, ushawishi, kuaminika kwake, ni ishara ya utendaji makini wa Serikali yake ukiungwa mkono na Taasisi za Kimataifa.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema Serikali ya Dkt Samia kutokana na juhudi za usimamizi thabit wa wa kisera, Serikali yake ikifikia malengo na shabaha za Kimataifa.
Mbeto alisema, Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu, aghalabu huharakisha utekelezaji wa miradi yenye ubora ya miundombinu, kupitia uwekezaji wa pamoja na kuongeza thamani ya fedha.
Aidha, alisema kutokana na utekelezaji wa mikakati ya kisera, Serikali ya Tanzania imekuwa ikivutia zaidi kutokana na kushirikisha mitaji ya sekta binafsi inayoimarisha Maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika.
“Mkakati wa Kuharakisha Ujenzi wa Miundombinu na kukamilisha miradi ya kimkakati kwa viwango. Kwa muktadha huo juhudi hizo na nyingine zinaibeba Tanzania mbele ya Mataifa mengine Afrika,” alisema Mbeto.
Pia, Katibu huyo Mwenezi alisema hatua ya Serikali ya Rais Dkt Samia, ikiwemo hatua ya kuvutia Wawekezaji, kuzishirikisha sekta binafsi na ya umma kwenye uwekezaji wa Nishati, Usafirishaji, na gesi Asilia, kunaipa heshima ya juu Tanzania.
“Baadhi ya wenzetu kwa kulazimisha umaarufu wa kisiasa hupotosha hata maendeleo yanayoonekana kwa macho. Ni kinyume na Tanzania inayotazamwa Kimataifa. Kupanda kwa thamani na matumizi ya rasilimali gesi na kumeimarisha Viwanda na Ajira,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, si hivyo tu, lakini pia kuonyesha Usalama wa Uwekezaji, kunafikisha ujumbe duniani kuwa Afrika ni eneo salama la kimkakati linaloshamirisha maendeleo kwa kasi.
Viongozi mbalimbali toka Mataifa ya Afrika wanahudhuria Mkutano katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo pia unahudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ya miundombinu, huku mgeni rasmi akiwa mwemyeji wake Rais Dkt. Samia.