Mbeto: Rais Dkt. Samia ni ‘Champion’ wa turufu za kisiasa

0

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi kimesifu uwezo mkubwa wa kisiasa alionao Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkakati wa kusaka turufu za kisiasa kuelekea ushindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.

Pia, CCM kimejigamba kuwa kina hazina kubwa ya wanasiasa wenye uwezo, vipaji, ufahamu na uzoefu katika medani za uongozi, diplomasia na siasa.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ameeleza hayo kufuatia uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro na kufanyika kwa mabadiliko madogo katika safu ya Sekretarieti ya NEC.

Dkt. Migiro amechukua nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Mstaafu Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ameteuliwa kuwa mgombea Mwenza wa Urais CCM.

Mbeto alisema, CCM ni chama kikubwa kinachojitegemea; kina mtaji wa nguvu na idadi ya wanachama wake, viongozi walioshiba uzalendo, uzoefu, upeo na amana katika jamii.

Akitaja kuteuliwa kwa Dkt. Migiro kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM, alisema ni kama kimbunga Hidaya kuelekea kukipatia ushindi chama hicho ifikapo Oktoba.

“Rais Dkt. Samia ni bingwa wa kusoma alama za nyakati katika kusaka piku na turufu za ushindi. Chama chetu kina hazina ya viongozi isiofilisika. Hakisubiri kuzoazoa mabaki yanayosazwa na wengine,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi, alisema uteuzi wa Dkt. Migiro kuwa Katibu Mkuu CCM ni ufunguo mpya utakaofungua kufuli za milango yote yenye kutu hatimaye kukipatia ushindi CCM usio na longolongo.

“Kwa wale wote wanaotaka kuitikisa CCM watakumbana na nguvu zake za asili. Nguvu za CCM ni zaidi ya tufani, kimbunga Tsumani. Tungependa wajue siku zote kina cha maji hakipimwi kwa kutumia kijiti au kutazama kwa macho,” alieleza.

Akifafanua zaidi, Mbeto alisema kelele zinazopigwa na baadhi ya mamluki wa kisiasa wasiolitakia mema Taifa letu zinasikika, lakini akasema majibu ya watu hao, yatajibiwa kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

“Nguvu na mtaji wa ushindi wa CCM hutokana na ridhaa ya watu. Kwa miaka yote CCM kimeshughulika na utatuzi wa changamoto za maendeleo ya watu. Watu wanakiheshimu , wanakitegemea na kukiamini,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here