Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema, hawapo tayari kuona kauli au vitendo vyovyote vitakavyohatarisha Muungano ambao umedumu kwa miaka mingi na ni moja ya tunu za Taifa.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, ambapo amesisitiza ikitokea wanaoshiriki kwenye jambo hilo ni miongoni mwa wanachama au viongozi wake, hatua za haraka zitachukuliwa dhidi yao.
“Muungano ni tunu, hatukuungana kwa kubahatisha, wakazi wa Zanzibar na wakazi wa Tanganyika, sote tunajulikana ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Muungano wetu huu haukuanza mwaka 1964, mwaka huko ulikuja Muungano wa kisiasa, ndio maana leo tupo na makabila yetu,” alisema Mbeto.
Akifafanua zaidi alisema, katika historia ya Zanzibar, Wamanyema waliolewa kwenye familia za hapa na wakapata watoto, hivyo ni jamii ambayo imekuja miaka mingi kabla ya Muungano.
“Kilichofanyika mwaka 1964 ni kuunganisha Muungano wa Kiserikali, ndio maana makabila yaliyopo Zanzibar, yapo Tanzania Bara, baada ya hapo wakaja Washiraz, wakaja watu kutoka India, Wareno, Wareno wapo hapa,”
“Wakaja ndugu zetu Waarabu wa Oman 1839, kwahiyo tuna mchanganyiko wa Mataifa mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa, pamoja na muingiliano huo, wazawa ni watu kutoka mwambao wa Afrika Mashariki na wameendelea kuishi kwa amani na utulivu na Muungano huo.
Mbeto alisisitiza kuwa, “Muungano huu ni wa kidamu, kidugu na kihistoria, tutaendelea kuudumisha, tunaendelea kuulinda, ndio maana viongozi wetu Rais Dkt. Samia na Rais Dkt. Mwinyi, wamekuwa wakihubiri Umoja na Amani ya Watanzania.”