Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapaswa kulaumiwa kwa kuwasaliti Watanzania.
Mbeto alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa habari, ambapo alisema Chadema walipaswa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili wapate nafasi ya kutoa maoni yao wakiwa bungeni badala ya mtindo wao wanaotumia hivi sasa wa kuzunguka mikoani.
Alisema, kitendo cha kususia uchaguzi, kimewakosesha uwakilishi ambao Watanzania walioupata kwa miaka ya nyuma, wakati bunge lilipokuwa na wabunge kama Tundu Lissu, Zitto Kabwe, David Kafulila na wengine, ambao waliibua mijadala mikubwa iliyoleta mtikisiko na mabadiliko kwenye nchi.
“Nakumbuka Waziri Mkuu alijiuzulu, ni kwasababu ya mawazo ya msingi ya wabunge hao. Serikali ilifanya mabadiliko mara ngapi kwa michango ya wabunge? Waliibua madudu mangapi Serikali ikachukua hatua? Hiyo ndo tunataka demokrasia iwe hivyo, sio kutukana,” alisema.
Aliendelea kusema “wanaleta siasa za chuki, matukio, tunataka wajenge watu wenye uwezo, akisimama mbunge unakubali, Serikali inasikia na inachukua hatua, Waziri Mkuu kwenye historia ya nchi hii alijiuzulu kutokana na hoja zilizoibuliwa na wapinzani, sasa unataka usikivu wa aina gani,?”
Alisema, wapinzani wanapaswa kushindana kwa hoja, na kuweka wazi kwamba alitamani kuona bungeni kuna wabunge zaidi ya 50 wa Chadema, lakini kwasababu ya uzembe wao, wamewagharimu watanzania ambao wanakosa kusikiliza mawazo mbadala.
“Leo unaacha kwenda kwenye jambo la msingi, unazunguka mtaani. Navishauri vyombo vya habari, viwashutumu Chadema kwa kuwakosesha Watanzania ladha ya mijadala bungeni, watanzania wanasikia,”
“Wangekuwemo mule bungeni, tungeona wanavyoibana Serikali, mikataba mingapi imefutwa bungeni enzi yao walipokuwepo akina Lissu? Miswada mingapi imebadilishwa? Watanzania tunapaswa kuwalaumu Chadema kwa kutoshiriki uchaguzi na kutowawakilisha vizuri kwenye maeneo yao,” alisema Mwenezi Mbeto.
Aidha, Mbeto alikiri kwamba, Chadema ina watu wazuri wanaojenga hoja na wasomi wazuri wakiwemo wachumi, lakini wameshindwa kutoa mchango kwa Taifa.
“Wapo nje, wanagombana na askari, wangekuwemo kwenye chombo cha kutunga sheria za nchi, chombo cha kupitisha bajeti ya nchi, hiyo bajeti inakwenda kuwatatulia watanzania matatizo yao, leo tungelikuwa wapi? Wakulaumiwa ni Chadema kwa kuwasaliti Watanzania,” alisisitiza Mbeto.