“Sasa najua ni nini ninapaswa kuangalia ninapojaza mafuta, kununua sukari au hata ninaponunua gesi ya kupikia.” Ni kauli ya Bw. Bilson Vedastus, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea Viwanja vya Chinangali Park, Dodoma.
Banda hilo limekuwa kitovu cha msongamano siku ya tatu ya maonesho, Juni 18, 2026 huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kujifunza jinsi Serikali kupitia WMA inavyohakikisha kila kipimo kinachotumika kibiashara na katika huduma ni sahihi. Maonesho yalianza tarehe 16 Juni na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Juni 2026.
Baada ya kupata maelezo ya hatua kwa hatua kutoka kwa wataalamu, wengi wameahidi kuwa mabalozi wa Wakala wa Vipimo katika maeneo yao.
“Tumeona jinsi pampu, mizani na vifaa vingine vinavyohakikiwa kuhakikisha vinapima kwa usahihi. Sasa hatuwezi kukaa kimya tukiona mteja anadhulumiwa. Tutawaeleza jirani zetu na kuripoti udanganyifu popote tutakapouona,” alisema Bi. Asha Siyaya.
Wataalamu wa WMA, Albogast Kajungu, Mbwana Amani na Said Ibrahim waliwaeleza wananchi kuwa uhakiki wa vipimo unagusa sekta zote zinazowahusu moja kwa moja kila siku. Katika sekta ya mafuta, pampu zote huhakikiwa na kuwekewa stika ya uthibitisho. Sokoni na madukani, mizani inayotumika kupimia sukari, mchele na mboga hufanyiwa ukaguzi ili mteja asipoteze pesa.
Sekta ya maji na umeme nayo haikuachwa nyuma. Mita za maji na umeme zinazotumika nyumbani na kwenye biashara ndogo huhakikiwa na kuthibitishwa ili kuhakikisha mteja analipia matumizi halisi na si makadirio au idadi isiyo sahihi. Vile vile mitungi ya gesi ya kupikia, bidhaa zilizofungashwa kama unga na sabuni, pamoja na mizani za barabarani zote huhakikiwa mara kwa mara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo, Bi Veronica Simba amesema lengo ni moja: kuhakikisha mwananchi anapata thamani kamili ya kila shilingi anayolipa, na amewahamasisha wananchi wengi zaidi kutembelea banda hilo kabla ya maonesho kuhitimishwa.