Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar , Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakuna mvutano wowote ndani ya chama hicho, kinachoendelea hivisasa ni chuki zinazotengenezwa na watu wenye mipango ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2030.
Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa habari na kuwataka Watanzania kupuuza propaganda hizo.
Mbeto alisema, kwenye mitandao ya kijamii, kuna watu wanasambaza madai kwamba kuna mvutano kati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wake Dkt. Emmanuel Nchimbi, jambo ambalo halina ukweli wowote.
Alisema, Makamu wa Rais ni msaidizi namba moja wa Rais na majukumu yake yametajwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akifanya majukumu mengine ambayo atapewa na Rais. “Usifikiri Makamu wa Rais anapokwenda sehemu hana mawasiliano na bosi wake.”
Alisema, kauli ya Dkt. Nchimbi aliyoitoa hivi karibuni kwenye Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) haikuwa na nia mbaya, badala yake imepotoshwa ili kutengeneza chuki.
Kwenye hotuba yake, Dkt. Nchimbi aliwataka Watanzania kuhakikisha wanapigania Katiba mpya kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia ambaye ana nia ya dhati ya kutekeleza suala hilo kama alivyoahidi.
“Nchimbi alisema, tumebahatika kupata Rais ambaye ana shauku na anataka Katiba mpya, kwa maana hiyo tuache vitu vidogo vidogo tukomae, tupambane tupate Katiba mpya, kwasababu Rais tuliyenae anataka Katiba mpya,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa, mbali na Rais Samia, chama nacho kinaitaka Katiba Mpya hivyo ni fursa muhimu.
Akifafanua zaidi alisema, kauli ya Nchimbi ililenga kuwahimiza Watanzania waione fursa hiyo katika mazingira ambayo Rais na chama kina msimamo mmoja, hivyo iwapo itapotea, wanaweza wasiipate tena.
“Kama unataka uhuru wa mahakama, Katiba mpya itaeleza, kama unataka tume huru ya uchaguzi, tutaipata kwenye Katiba mpya, kama unataka uhuru wa kujieleza, haki za binadamu, haki zote utazipata kwenye Katiba mpya,” alisema.
Aliendelea, “ndio maana Makamu wa Rais akasema, tupambane tupate Katiba mpya ili yale yote tunayoyahangaikia tukikomaa tutayapata iwapo tutampa ushirikiano Rais, kwa hiyo sioni tatizo kwenye kauli yake, amesimamia msimamo wa bosi wake Rais Samia ambaye aliahidi kwamba tutapata Katiba mpya.”
Alisema, kauli hizo zimepotoshwa kwa makusudi kwa ajili ya kugombanisha watu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2030 “watu wanataka kupandikiza chuki kwa kuunganisha mambo, mi najua hii ni homa ya 2030, watu wanataka kugombea nafasi.”
Mbeto alisema, watendaji wote wanafanya kazi kufuata maelekezo na taratibu za chama na wana utaratibu pale wanapoona kuna jambo, lakini kwasasa hali ni shwari hakuna tatizo lolote. “Niwatoe wasiwasi watanzania, nchi ipo shwari, Makamu wa Rais anafanya kazi zake kwa maelekezo ya Rais.”