Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mpinduzi (CCM) kimesema kama wakati ambao Rais Ali Hassan Mwinyi alipoachiwa uongozi na Mwalimu Julius Nyerere Mwaka 1985, hakurithi urais tu, bali pia alibeba jukumu la kujenga nchi yenye Umoja na uaminifu.
Aidha, ndivyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoichukua nchi toka kwa wenzake waliomtangulia na kuifikisha katika haiba ya maendeleo yanayoonekana sasa.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar , Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akisifu juhudi na uongozi wa Rais Dkt. Samia tokea aingie madarakani.
Mbeto alisema, kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyoipa heshima Tanzania duniani kote, kwa kuwa huru na utambulisho wake kisiasa kupitia siasa ya Ujamaa na kujitegemea, ndiyo kazi inayoendelezwa na Rais wa Awamu ya sita.
Alisema, kwa kufuata nyayo zile zile na kama kila kiongozi alivyoondoka madarakani kama alivyofanya muasisi wa Taifa la Tanzania, na waliomfuatia baadae wote wamerithi wakipita njia yake.
“CCM ni chama cha siasa mfano Barani Afrika na duniani kote. Si kwa upande wowote wa Jamhuri ya Muungano ametokeza Rais aliyetaka kuongeza muda wa kubaki madarakani akafanikiwa,” alisema Mbeto.
Kadhalika Katibu Mwenezi huyo ameeleza kuwa , wakuu wote wa nchi baada ya Mwalimu Nyerere, wameendeleza aina ile ile ya siasa yetu, diplomasia ya kiuchumi na uhusiano wa Kimataifa.
“Ni fahari ilioje kwa Rais Samia kualikwa Angola kuzindua hospitali ya Rufaa iliopewa jina la Mwalimu Nyerere. Ziara hiyo imeithibitishia dunia thamani ya mchango wa Tanzania na kuheshimika jina la Mwalimu Nyerere,” alieleza Mbeto.
Pia, Mwenezi huyo aliongeza kusema hivi karibuni Rais Dkt. Samia akiwa nchini Urusi, aliihakikishia dunia kuwa Tanzania ni rafiki na mshirika wa Mataifa yote duniani isiofungamana na siasa ya upande wowote.
“Taifa letu ni huru na uhuru wake umetumika kuwanufaisha wengi duniani. Tumepinga ubaguzi wa aina yoyote huku tukipigania haki za binadamu bila kuyumba. Tutalinda heshima hiyo na kujivunia,” alisisitiza Mwenezi huyo.
Akizungumzia upande wa Zanzibar, Mbeto alisema vipindi vyote vilivyotangulia vimetimiza wajibu na kuivusha kiuchumi Zanzibar hadi mahali ilipofikia.
Hata hivyo, alimpa sifa nyingi Rais wa Awamu ya Nane Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuiendeleza Zanzibar na kuleta mageuzi makubwa ya kisiasa na Kiuchumi.