Mbeto amtajia OMO sababu za CCM kukaa madarakani kwa muda mrefu

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman (OMO), kutoulinganisha uimara wa CCM na vyama vingine Barani Afrika kwakuwa CCM ndio baba wa demokrasia chenye Amana na Nguvu za ushawishi kisiasa katika jamii.

Pia, CCM kimeelezea karibu Vyama vyote vya Siasa Kusini mwa Jangwa la Sahara vimejifunza mbinu na mikakati ya ukombozi, kupigania uhuru na Siasa safi kutoka CCM.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ta Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis aliyemtaka Othman (OMO) kuijua historia ya CCM na michango yake kwa nchi kadhaa za Afrika.

Mbeto alikuwa akijibu mapigo kutokana na madai ya OMO kuwa katika nchi kadhaa za kiafrika Vyama vya Ukombozi vimeondolewa madarakani kupitia Uchaguzi na kukubali matokeo lakini CCM hakitaki .

Akijibu hoja hizo, Mbeto alisema si kwamba CCM hakitaki kuondoka bali kina nguvu kubwa za kisiasa ndizo zinazokifanya hicho kiendelee kuaminiwa na wananchi na kupigiwa kura kwenye chaguzi kuu zote .

“CCM hakipo madarakani kwa kujiweka kwa shuruti . Hakiongozi kwa muda mrefu ila wananchi ndio wanaotaka kiendelee kubaki madarakani kwa sera zake, uaminifu na historia yake adilifu,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alieleza kuwa Vyama vyote vya Kisiasa havikujijenga ndani ya umma mara baada ya kupata uhuru kama TANU/ASP na CCM vikiweza kujiimarisha.

“CCM kina mizizi usioweza kukatika kirahisi hata baada ya miaka hamsini toka sasa. Kimeutumia vyema mfumo wa chama kimoja na kushika hatamu za utawala kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kuifananisha CCM na Vyama vingine ni kukikosea adabu,” alieleza.

Mbeto alisema, tofauti iliyopo kati ya CCM na vyama vingine ikiwemo na vyama vya upinzani vya Tanzania, CCM kimeendelea kuungwa mkono kwa sera zake za kulinda Umoja, Amani, mshikamano na maendeleo.

“Hakuna Seychelles, Afrika Kusini huru , Botswana, Lesotho, Angola, Msumbuji, Zambia, Malawi, Namibia bila Tanzania chini ya CCM. CCM ndio mkufunzi wa siasa, maendeleo ya demokrasia na umoja wa Kitaifa,” alisisitiza.

Mbeto akieleza zaidi, alimtaka Othman ambaye ni Makamo wa Kwanza wa Rais SMZ, kutokiona CCM ni chama kidogo akakifananisha na ACT, Chadema au CUF ambavyo vimeundwa kati ya mwaka 1993 na zaidi ya mwaka 2000.

“Si kwamba CCM kipo madarakani kwa muda mrefu bali kinawekwa kwa hiari ya wananchi wenyewe kwa muda mrefu. OMO atofautishe kuwekwa na kujiweka,” aliongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here