Matumizi ya Teknolojia yaongeza ufanisi na tija TANAPA

0
Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, Mussa Nassoro Kuji Juma, akizungumza katika mkutano baina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ikiwa ni mfululizo wa program ya kuelezea mafanikio ya taasisi na mashirika ya umma katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita (Picha na Francis Dande).

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limejikita katika matumizi ya teknolojia mbalimbali ambayo yamesaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kila siku.

Kamishna Mkuu wa Uhifadhi Mussa Kuji alisema hayo kwenye mkutano na Waandishi wa Habari na Wahariri uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina.

Akitaja baadhi ya huduma ambazo zinatolewa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ni pamoja ukusanyaji mapato kwa njia ya Kidigitali kwa kuanzisha “online reservation and booking system.”

“Tumeanzisha mfumo wa kufanya malipo ya vibali vya kuingia hifadhini yaani “e-permit” ambao unamuwezesha mtalii kufanya malipo akiwa sehemu yoyote ile duniani kabla hajaingia hifadhini,” alisema Kuji.

Mbali na huduma hiyo, alisema wameanzisha matumizi ya ‘smart gates’ katika hifadhi ya Serengeti, Tarangire na Ziwa Manyara kwa lengo la kuongeza udhibiti wa mapato, huku wakianzisha mfumo wa ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wateja kuhusu utoaji wa huduma (online customer feedback).

“Tumeimarisha ulinzi wa wanyamapori kupitia teknolojia ya “Low Range Wide Area Network” (LoRa WAN) yenye uwezo wa kuona eneo kubwa la hifadhi. Tumeimarisha matumizi ya mifumo ya taarifa za Kijiografia.”

“Mifumo hii inasaidia kuongeza ufanisi katika doria za kuzuia ujangili. Vile vile tumeongeza matumizi ya ndege nyuki (drones) kwenye kuimarisha ukaguzi wa maeneo ya Hifadhi za Taifa,” alisema Kuji na kuongeza kuwa, matumizi hayo ya teknolojia ya kisasa yameongeza tija kwa kuwezesha ukaguzi wa maeneo makubwa ndani ya muda mfupi.

Katika hatua nyingine, Kamishna Mussa Kuji alisema, Shirika hilo limeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa linabuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vitaliingizia fedha na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Alitaja baadhi ya vyanzo hivyo bunifu vya mapato ambavyo vimeendelea kuibuliwa na Shirika; kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika (TANAPA Investment Limited – TIL) inayolenga kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na pia kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Shirika kwa kutekeleza miradi mbalimbali.

Kampuni hiyo itaendesha kiwanda cha ushonaji wa sare za watumishi na kupokea tenda kutoka taasisi nyingine, itasimamia Hoteli yenye hadhi ya nyota tatu katika eneo la Rubambagwe Wilaya ya Chato yenye vyumba 30 vya kulala, ambayo inaelezwa ujenzi wake umefika asilimia 67%.

Alisema, lengo la kujengwa kwa hoteli hiyo ni kufungua ukanda wa Magharibi kwa upande wa Utalii, ikizingatiwa kuna hifadhi Burigi Chato na nyinginezo, hivyo kuna haja ya kuwa na hoteli kwa ajili ya kuwapokea wageni wanaofika kutembelea vivutio vilivyopo kwenye ukanda huo.

Aidha, Kuji alisema wamebuni ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa hadhi ya Kimataifa wenye mashimo 18 uliopo eneo la Forti Ikoma – Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Hata hivyo, Kuji alisema wataendelea kusimamia jukumu la kuhifadhi maliasili zote na kutunzwa kikamilifu wakati wote. “Ulinzi wa maliasili, usalama wa watalii, usalama wa watumishi wa TANAPA, na usalama wa wawekezaji utaendelea kuimarishwa wakati wote ili kuhakikisha kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania zinaendelea kuwa ni maeneo salama na sahihi kwa watalii na wawekezaji.”

Pia, aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo yaliyoainishwa katika Hifadhi za Taifa kwa nia ya kuboresha huduma za malazi kwa wageni, sambamba na uwekezaji, “nitoe wito wa watanzania kutembelea hifadhi zetu kwa ajili ya kujivinjari na kupumzika. Uboreshaji huu na kutembelea hifadhi utawezesha Serikali kufikisha watalii Milioni 5 na mapato ya Dola za Kimarekani Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here