Matibabu kwa njia ya masafa, ndiko dunia inapoelekea

0

Na Dkt. Raymond Mgeni

KATIKA mpango mkakati wa maendeleo endelevu ya Dunia wa mwaka 2030 ni kuhakikisha mifumo bora ya afya na kumsaidia kila mmoja kupata huduma nzuri za kiafya.

Afya ni lengo namba tatu mojawapo katika malengo 17 ya malengo mkakati wa maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Dunia. Lengo ni kuwa kila mmoja ana nafasi ya kupata huduma bora za kiafya.

Lengo hili linahimiza watu mbalimbali duniani kubuni mifumo wezeshi ya utoaji huduma bora za afya, kuimarisha miundombinu, ujenzi wa vituo vya afya, kuimarisha mifumo ya kitafiti na vitengo vyote shiriki kuimarisha afya mfano madawa, maabara na kadhalika.

Katika juhudi zote hizo, zimesaidia nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuona pana umuhimu mkubwa wa TEHAMA katika utoaji wa huduma za afya na hili limejitokeza kwa kuona watu wengi siku hizi wana uwezo wa kupata huduma za Kidijitali.

Si tu huduma za pesa kupitia mtandaoni kama Tigopesa, MPESA, Halopesa na kadhalika ila hata huduma za kiafya zinawezekana kuwa katika mifumo ya Kidijitali.

Dunia inaenda kasi na inaonesha namna teknolojia ya mawasiliano inavyoenda kuleta mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma za kimatibabu kwa mfumo wa TEHAMA, ingawa bado ni elimu ngeni kwa watu kuelewa mfumo huu wa Kijidijitali wa kuwasiliana na Mtaalamu wa afya na ukapata ushauri na matibabu.

Ila katika jamii zetu imekuwa kawaida kwa watu kuwapigia simu madaktari na kuomba ushauri au hata kuandikiwa dawa wakanunue. Zipo athari za kufanya hivyo kiholela.

Ila mfumo huu wa huduma ya kuwasiliana na mgonjwa kwa simu unaporasimishwa na kwa namna vituo maalumu vitakavyokuwepo itasaidia watu wengi ambao hutamani kujua huduma hizi kuzipata bila vikwazo vyovyote vile. Si wakati wote watu hupendelea kwenda hospitali na kuhangaika na foleni kubwa wanaposubiria huduma kwa daktari.

Mfumo huu wa Kidijitali unahitaji mifumo mizuri ya mawasiliano na mtandao mkubwa wa madaktari katika kuwa na mawasiliano, ambapo mgonjwa anaweza kuwasiliana haraka tu kujielezea dalili na pia kupanga miadi kama patakuwa na uhitaji wa kwenda kumuona moja kwa moja.

Mfumo huu unapunguza gharama ambazo mtu huzipata akienda moja kwa moja katika hospitali. Mtu anaweza kulipia kidogo tu gharama ya ushauri na kupewa maelekezo ya kimatibabu. Dunia ndo inakoelekea huku kwa kuanza kuwahudumia wagonjwa wakiwa nyumbani kwa njia za Kidijitali.

Gharama za kutoka eneo la hospitali moja kwenda hospitali nyingine ni kubwa na huenda inachangia wagonjwa kuchelewa kupata huduma katika muda unaotakiwa, maana wengine hadi wajipange kutafuta nauli au pesa za matibabu; hali ya mgonjwa inazidi kuwa mbaya.

Hili linachangia baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha wakiwa bado hawajapata huduma kutokana na hali ngumu za kugharamia matibabu. Mfano, mgonjwa ambaye kapewa rufaa kwenda kuonana na madaktari bingwa hospitali za Kanda au Taifa huwa ni mtihani kwao.

Ila vipi ikitokea kuwa na mfumo wa Kijiditali ambapo kabla ya kuonana na daktari anaweza kuwasiliana na daktari moja kwa moja na akapata huduma za maelekezo na matibabu akiwa mbali?

Haya yameshaanza katika nchi nyingi duniani hasa zilizoendelea, ambapo wagonjwa wana mawasiliano na madaktari na wanapopata dalili zozote za ugonjwa wana nafasi ya kuongea na madaktari na kupata matibabu.

Mfumo huu umeanza kusaidia hata mtu kuwa na vifaa vya Kielektroniki kama saa za kuvaa ambapo mtu anaweza kupata nafasi ya kujua hali zake za kiafya kwa vipimo kama kujijua hali ya presha ya damu, hali ya joto la mwili na kadhalika.

Hata wakati mwingine vifaa hivi vinaweza kumsaidia mtu kumpa taarifa mbalimbali za kiafya kwa haraka. Teknolojia ndivyo inavyoenda kuleta mapinduzi makubwa katika miaka inayokuja.

Juhudi ya Serikali kufikiria kuwa na vituo vya matibabu ya masafa marefu (telemedicine center) kutokana na kiasi cha pesa zilizotoka Shirika la Fedha duniani itaibua uelewa mkubwa wa makundi mbalimbali kwa kuanzia na watu wa kada ya afya na watu wote watakaokuwa wakihitaji huduma za matibabu na ushauri za masafa marefu.

Hatuwezi kukwepa mabadiliko ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma na hili linajitokeza kidogo kidogo ambapo hospitali za serikali, binafsi au taasisi za kidini kwa kuanzisha kurasa za mitandao ya kijamii kujiunganisha na wateja wao, utoaji wa elimu ya afya, taarifa mbalimbali za mabadiliko ya kihuduma.

Hili linaonesha namna mfumo huu utakuja kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma bora kwa jamii na taifa miaka ijayo. Ni wakati sasa ambapo sekta ya afya inahitaji kujiandaa na kuweka maandalizi ya kuandaa wataalamu wa kada hii ya afya kukabiliana na mabadiliko haya.

Mfumo wa TEHAMA katika sekta ya afya utasaidia kuepusha matatizo mengi ya kiafya ambayo hujitokeza na yangezuilika mapema yasiwe na athari kwa watu kwa uwepo wa mifumo ya haraka ya mgonjwa au ndugu wa mgonjwa kuwasiliana na mtaalamu wa afya moja kwa moja kabla ya kwenda kupata huduma zaidi hospitalini.

*Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu wa Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya, Idara ya Afya ya Akili, anapatikana kwa Simu:+255 676 559 21, barua pepe: raymondpoet@yahoo.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here