Mapinduzi ndio heshima, utu na umoja wetu

0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika uwanja wa Amaan Januari 12, 2024.

Na Dkt. Juma Mohammed

JANUARI 12, 2024 Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yametimiza Miaka 60. Wakati tukifika tamati ya sherehe hizo, kamwe hatuwezi kuyaweka katika kaburi la sahau majina ya wazalendo waliojitoa kuikomboa nchi kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kisultan kutoka Oman.

Jemedari, Rais wa Afro Shirazi Party, Sheikh Abeid Amani Karume na wenzake. Hatuwezi pia kumsahau, Mwenyekiti wa Afro – Shirazi Party – Youth League, Kanali Seif Bakari Omar ambaye ushupavu wake uliwatia ari na nguvu ya kutekeleza bila woga Azimio la kumng’oa Sultan na vibaraka wake.

Kanali Seif Bakari Omar, aliongoza Kamati ya Watu 14 Vijana wa A.S.P. waliowaongoza wananchi wengine kumfurusha Sultan Januari 12, 1964. Suala la kuyalinda Mapinduzi haya ni jambo lisilokuwa na muhali hata kidogo kwani ndio heshima na utu na umoja wetu.

Ukiacha sababu za kisiasa, lakini pia kulikuwa na sababu za kijamii ambazo ziliwasukuma Wazalendo wa Zanzibar kufanya Mapinduzi ikiwemo hali duni ya maisha, ukosefu wa huduma muhimu katika sehemu kubwa ya nchi na mambo mengine ambayo hayakuwafurahisha wananchi walio wengi.

Wanyonge Waafrika walio wengi walikuwa wakiishi katika vibanda vya udongo vilivyoezekwa makuti au madebe ya mabaki ya mafuta na vipande vingine vinavyofanana na bati.

Sehemu za Ng’ambo, mashamba ilikuwa na vibanda vya kukandika kwa udongo na kuezekwa au kufungwa makuti na ilikuwa ikikaliwa na wanyonge Waafrika ambao maisha kwao yalikuwa ni yenye mashaka na dhiki maana wakati wa masika na mvua za vuli hawakuwa wenye furaha.

Katika kipindi chote cha Utawala wa Kikoloni wa Kisultan kutoka Oman, miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakiwapa tabu na kuwasononesha; ni suala la makazi bora.

Walikuwa katika hali mbaya wakilala katika vibanda vibovu wakinywa maji ya kuokota wakibeba mizigo mizito kwa ukosefu wa barabara ya kuchukulia mazao yao, nishati ya umeme haikuwa kama ilivyo leo, huduma za afya hazikuenezwa sehemu zote na zilitolewa kwa matabaka.

Katika zama kabla ya Mapinduzi, Mji wa Unguja, uligawiwa sehemu mbili; Mjini nyumba za mawe matupu na sehemu ya ng’ambo ya nyumba za udongo. Sehemu ya mjini iliyokuwa na nyumba nzuri ikikaliwa na Sultan na jamaa zake, Mabepari na Mabwanyenye, Makabwela waliselelea Ng’ambo na Mashamba.

Kwa hakika, Zanzibar ya kabla ya Mapinduzi ni tofauti sana na Zanzibar ya leo ambayo kila mwenye macho haambiwi tazama, Zanzibar imepiga hatua kuanzia miundombinu ya barabara, elimu, huduma za kijamii na hata siasa.

Kama watu waliofariki miaka ya mwanzoni mwa Hamsini na mwanzoni mwa Sitini mambo kwao leo ni tofauti na pengine hawataamini kuona mji ulivyopambwa na nyumba za kisasa mjini na mashamba.

Ukienda Bambi, Makunduchi, Chaani, Kilimani, Kikwajuni, Chake Chake, Mkoani, Wete utaona nyumba za maendeleo zilizojengwa na SMZ ambazo Wakwezi na Wakulima wanaishi humo katika nyumba zinazostahiki kukaa binadamu aliye huru katika nchi yake.

Kwa upande wa utawala bora, miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar tumeshuhudia kutandikwa misingi ya haki na usawa kwa jamii kwa kuifanyia kwanza marekebisho, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo iliweka mfumo bora zaidi katika uendeshaji wa Mahakama na kuanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

Marekebisho ya Tisa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yaliyofanyika mwaka 2002, yalihusu kuanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambapo chini ya marekebisho yale sasa kazi ya kuendesha mashtaka imekuwa chini ya usimamizi wa DPP na sio Polisi.

Marekebisho ya Nane ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2002, ilihusu zaidi kuwa na Tume huru ya Uchaguzi ambapo pia ilianzisha Daftari la kudumu la wapigakura badala ya mabuku ya karatasi ya mchele yaliyokuwa yakilalamikiwa, kutumia kitambulisho katika uchaguzi na sheria hiyo iliweka uwanja sawa katika uchaguzi.

Zanzibar imeingia kwenye orodha ya nchi zenye Tume Huru ya Uchaguzi kama ilivyopendekezwa katika Muafaka wa kisiasa wa CCM na CUF wa Oktoba 10, 2001.

Kwa dhamira ile ile ya kuendeleza malengo ya Mapinduzi, Mwaka 2010, SMZ ikawasilisha katika Baraza la Wawakilishi muswada wa sheria ya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yaliyoanzisha kura ya maoni na kuweka mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa hivyo, kutulia kwa hali ya kisiasa Zanzibar na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni matukio makubwa mawili ambayo yanatufanya kuwathibitishia walimwengu mafanikio ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Ijapokuwa kuna changamoto kadhaa, lakini changamoto hizo haziwezi kufuta ukweli wa mafanikio haya na mengine mengi. Hivyo, tuna kila sababu kujivunia na kuendeleza misingi ya Mapinduzi.

Je, tutaendelea kuyalinda Mapinduzi au tutawaacha wanaobeza mafanikio ya kujitawala kwa kuwakumbuka mashujaa wetu kwa wimbo mzuri uliopangika kwa beti zake au kwa kurejea dhamira ya waasisi wale wa Mapinduzi walipojitolea roho zao na mali zao kupigania maslahi ya nchi yao dhidi ya Ukoloni?

Je, vijana wa leo wanaelezwa nini kuhusu Mapinduzi hayo, wanafahamu nini dhamira yake? Bila shaka kipimo cha ushupavu katika kusimamia kwa vitendo malengo ya Mapinduzi kinatakiwa kiwekwe wazi na kila mtu awe tayari kutetea na kuendeleza Mapinduzi kwa nia ile ile ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Ni wajibu wetu kuthamini ujasiri wa vijana ndani ya ASP ambao haukuwa na mfano, wazee pia nao hawakupenda kuwavunja moyo vijana wao na kwa msingi huo waliona kwamba kuendelea kutawaliwa na mkoloni Sultan ni kukisaliti kizazi kijacho ambacho ndio tunasherehekea Miaka 60 kwa kutembea kifua mbele katika nchi huru.

Kwa hakika kizazi cha leo hakitakuwa kimesamehewa na waasisi wa Mapinduzi ikiwa hawatoendeleza na kusimamia kwa dhati malengo ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here