London, UINGEREZA
MALKIA Elizabeth II wa Uingereza amefariki hivi karibuni, na kuelezwa kuwa ni alama za mwishoni za urithi wa ukoloni Duniani.
Utawala wa mama huyo ni wa muda mrefu wa miaka 70 kutoka 1952 hadi 2022, ambao nusu yake ulitumika kupambana na wapigania uhuru waliokandamizwa na taifa hilo la Ulaya Magharibi.
Wachambuzi wanasema, Mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza, yalikuwa yakiendesha vita vya kujikomboa kutoka utawala kandamizi wa London chini ya Malkia Elizabeth II.
Hivyo, wanasema, jina lake ni alama inayokumbusha urithi wa ukoloni wa nchi hiyo duniani, ambao ulidumu kwa mamia ya miaka.
Nalo Shirika la Habari la ‘Pars Today’, katika uchambuzi wake, linasema kwamba, mwenendo wa ukoloni wa Uingereza ulianza kwa upanuzi wa jeshi lake la wanamaji katika karne ya 16, na taratibu ukaenea katika pembe zote za dunia kutoka Asia hadi Oceania, na kutoka Afrika hadi bara Amerika.
“Kwa kadiri kwamba kabla ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia, ukoloni wa Uingereza ulikuwa imefikia upanuzi wake wa juu zaidi” linaeleza.
Kimsingi, wachambuzi wanafafanua kuwa, ufalme wa Uingereza ulijumuisha, makoloni, milki na maeneo yaliyokuwa chini ya himaya ya muungano wa ufalme mkubwa wa Uingereza, ambao msingi wake ulianza kuwekwa katika karne ya 16 na kuendelea hadi mwishoni mwa karne ya 20.
Historia inafichua kuwa, mwaka 1922, eneo lililokuwa chini ya himaya ya Uingereza lilifikia zaidi ya kilomita mraba milioni 33, na idadi ya watu wa ufalme huo kufikia zaidi ya watu milioni 450.
Hivyo, ufalme wa Uingereza ulitawala zaidi ya robo ya ardhi ya dunia na robo ya idadi ya watu wote duniani wakati huo.
Mataifa yaliyokuwa chini ya utawala huo wa kikoloni yalitapakaa katika pembe zote za dunia na ndio maana ya kauli mashuhuri inayosema kwamba “jua huwa halitui kwenye ufalme wa Uingereza.”
Ukoloni wa Uingereza unaweza kusemekana kuwa, ulianza katika karne ya 16 kwa kuanzishwa Kampuni ya India Mashariki mnamo 1599.
Kampuni hiyo iliimarisha misingi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza katika maeneo yenye rutuba ya Asia Kusini, na kuanzia wakati huo, shughuli zote za kikoloni na kibeberu za Uingereza katika mataifa ya Asia Kusini zikawa zinatekelezwa kupitia kampuni hiyo.
Wachambuzi wanasema, ushawishi mkubwa na utawala wa Uingereza juu ya India, karne tatu baada ya kuanzishwa kampuni hiyo, ulipelekea India kutangazwa kuwa sehemu ya milki ya Uingereza, hivyo Malkia Victoria akatawazwa kuwa mkuu wa dola la India na Uingereza.
Zama hizo, wanafafanua kwamba, zinachukuliwa kuwa zama za Uingereza kufanya uporaji mkubwa wa utajiri na maliasili za watu wa India, ambapo kupitia visingizio vya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, Uingereza iliimarisha pakubwa ushawishi wake wa kisiasa katika nchi hiyo ya bara Asia.
wa ujumla, India inaweza kuchukuliwa kuwa koloni muhimu zaidi la Uingereza katika kipindi hicho hadi wakati wa kujipatia uhuru wake mnamo 1947.
Mwenendo wa ukoloni wa Uingereza katika hatua za baadaye, ulipanuka kwa kasi kwa kutekwa maeneo muhimu katika eneo la Amerika ya Kaskazini na Bahari ya Karibian, bara Afrika, Asia Magharibi na Asia Mashariki na Oceania, ambapo ni nchi chache mno zilizokuwa na uwezo wa kukabiliana na uvamizi wa moja kwa moja wa London.
Mmoja wa wachambuzi hao Stuart Laycock anasema kati ya nchi 200 duniani, ni 22 tu ndizo ambazo hazikuvamiwa na Uingereza.
“Uingereza ilipewa jina hilo wakati wa utawala wa Malkia Victoria, ambaye kwa kiburi kikubwa alisema kuwa, kwenye ufalme wake jua huwa halitui.” anabainisha.
Anasema, athari za upanuzi huo wa kikoloni ni nyingi kuliko inavyoweza kuonekana kwenye ramani za kijiografia, kwa sababu nchi nyingi zilishambuliwa kijeshi na Uingereza na hatimaye kufanywa makoloni yake rasmi.
Ukoloni wa Waingereza katika maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wake, unaelezwa kuwa, uliandamana na vitendo vya ukatili, ukandamizaji mkubwa wa wenyeji, utumwa wa Waafrika, uporaji mkubwa wa maliasili, matumizi mabaya ya nguvukazi ya wakoloniwa na vitendo vingine vingi visivyo vya kibinadamu.
Mchambuzi mwingine Ghulam Ali Haddad Adel, Mkuu wa Chuo cha Lugha na Fasihi ya Kiajemi cha Iran anasema kuwa, hakuna sehemu yoyote duniani iliyoepuka ukoloni wa Uingereza, na hata Marekani ya sasa iliwahi kuwa koloni la Uingereza.
Jambo muhimu ni kwamba, juhudi za kupambana na ukoloni wa Uingereza bado zinaendelea katika maeneo ambayo yangali yanadhibitiwa na nchi hiyo ya Magharibi.
Kuhusiana na suala hilo, wanasiasa na wanaharakati wa makoloni ya zamani ya Uingereza katika eneo la Caribbean, kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II na kuanza utawala wa Charles III, kwa mara nyingine tena wanasisitiza matakwa yao ya kuondoka katika udhibiti wa ukoo wa ufalme wa Uingereza, na kulipwa fidia ya utumwa waliofanyiwa na London.
Mataifa ya Jamaika, Antigua na Barbuda katika eneo la Caribbean, ambazo hata baada ya kujitoa katika utawala wa ukoloni wa moja wa moja wa Uingereza, bado ziko ndani ya mfumo wa Jumuiya ya Madola, zinataka kujitoa katika mfumo huo katika karne hii ya 21 kwa kuamini kuwa, kuwemo humo ni kuendeleza ukoloni mamboleo wa Uingereza.