WAZIRI Mkuu Kasimu Majaliwa amehutubia Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) na kusema Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ni msingi wa matumaini katika kukabiliana na changamoto za kidunia.
Hii ni mara ya pili kwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo mara ya kwanza ilikuwa Septemba 27, 2010 wakati Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Kayanza Pinda alipolihutubia Baraza la 65 (UNGA65).
Ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Septemba 27, 2024) wakati akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka huu wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Nchi mbalimbali za dunia jijini New York, Marekani anakomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Tanzania imedhamiria kufanikisha malengo endelevu ya kiuchumi, ufugaji, uwekezaji katika miundombinu na mifumo ya kidijitali, uvuvi na nishati.
“Lengo letu ni kufikia uhakika wa kupunguza umasikini, kutengeneza ajira mpya na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi shirikishi katika nyanja mbalimbali,” alisema na kuongeza kwamba kuna shuhuda nyingi za taarifa za makuzi katika sekta hizo nchini Tanzania zinazotokana na mikakati kama ya Kesho Iliyo Bora (BBT) unaohusu kilimo kwa Tanzania Bara na uwezeshaji wanawake wanaoshiriki kilimo cha mwani Zanzibar.
Alisema, Tanzania kama yalivyo mataifa mengine, imekuwa ikipambana na changamoto kama za athari za ugonjwa wa uviko (COVID 19), kwenye sekta ya afya, mabadiliko ya tabianchi yanayojidhihirisha katika ongezeko la hali mbaya ya hewa kama mvua haribifu na ukame uliokithiri, pamoja na mambo mengine, vimeathiri ufikiwaji wa malengo endelevu.
Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia pia Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje kuhusu utu, kwamba Desemba 14, 1961, wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Msingi wa matendo yetu, ya ndani (ya nchi) na ya nje (nchi za nje) utakuwa ni kujaribu, kiungwana, kuheshimu utu wa mtu.”
Alisema, Tanzania imeendelea na msimamo huo katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi na kwamba kwa muktadha huo Tanzania ilikuwa ni mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika (OAU) ikiwaunga mkono wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali ya Afrika.
Alisema, pamoja na kupatikana kwa uhuru, mataifa hayo bado yanakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na mazingira hatarishi kwa utu yanayokwamisha upatikanaji wa maendeleo halisi. “Kwa hiyo tunatoa wito watu wajitawale wale ambao bado katika mifumo ya ukoloni, na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa mataifa ya Cuba na mengineyo.”
Alitumia jukwaa hilo kuliarifu Baraza hilo juu ya uwepo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika nchini. “Novemba mwaka huu (2024), Tanzania itafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kisha kufuatiwa na uchaguzi wa Rais na Wabunge Oktoba, 2025.”
” Tunapojiandaa kwa matukio haya ya uchaguzi, ningependa kuliarifu Baraza hili kuwa demokrasia, haki za binadamu, na utawala wa sheria vitaheshimiwa, sambamba na maono ya Rais Samia kama ilivyoelezwa katika falsafa ya 4Rs, ambazo ni upatanisho, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi upya.”