Na Julieth Laizer, Arusha
MATUKIO ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanaendelea kushika kasi kutokana na wazazi wengi kutokuwa na muda na watoto hali inayowafanya watoto kujiingiza kwenda mambo yasiyofaa na kufanyiwa ukatili zaidi.
Aidha, hali ya ukatili wa watoto kwa sasa hivi inaelezwa kuwa mbaya na hiyo ikichangiwa na wazazi wenyewe kutokuwa na muda na watoto, hivyo watoto kukosa elimu ya makuzi yaliyo bora na hivyo kusababisha kufanyiwa ukatili.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini, Mwantum Mahiza wakati akizungumza katika kikao maalumu cha wadau wanaojihusisha na masuala ya watoto jijini Arusha.
Mahiza alisema, kwa sasa watoto hawapo salama, kwani wanafanyiwa mambo ya ajabu na ya kutisha na wanaofanya hivyo ni ndugu wa karibu jambo ambalo linawafanya watoto wakose amani hata ya kukaa kwenye familia zao.
Alisema, watoto wanafanyiwa ukatili kwa kiwango kikubwa, hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya watoto kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kutoa elimu kwa jamii kuhusu makuzi na malezi na maadili.
“Mifumo iliyopo kuanzia ngazi za chini ikitumika vizuri itasaidia kuzuia maswala ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa watoto, kwani huko ndiko sehemu sahihi watoto wataweza kuripoti matukio wanayofanyiwa kwa urahisi zaidi na kuchukuliwa hatua za kisheria mapema.” alisema Mahiza.
Aidha, ametaka vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto kushirikishwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa mila, viongozi wa dini katika ngazi zote ili kwa pamoja waweze kuongeza nguvu ya kukemea na kudhibiti matukio hayo, kwani hali ya watoto kwa sasa ni mbaya na ukatili umekithiri.
Kwa upande wa Kaimu Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’S) , Mussa Sang’anya alisema suala la ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni changamoto kubwa, hivyo nguvu zaidi inatakiwa kuongezwa kwa Mashirika na hata wadau mbalimbali ili kwa pamoja kushirikiana katika kukemea matukio hayo.
“Leo tumekutana hapa na ni kikao kazi cha pamoja kuhakikisha kila mmoja wetu anakuja na maazimio na mikakati ya kufanya katika kudhibiti suala la ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wetu na sisi kama Wizara tutaendelea kutoa miongozo mbalimbali kuhakikisha watoto wanakuwa salama kila wakati,” alisema.
Aidha, ameyataka Mashirika binafsi yanayotetea haki za watoto kuwa na nia moja ya dhati katika kusaidia watoto kupata haki zao na kuhakikishausalama wa mtoto unaendelea kulindwa na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana kwa ajili ya watoto zinasambaa nchi nzima ili wote wapate huduma.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la kutoa malezi kwa watoto SOS Tanzania, David Mulongo alisema, wamekuwa wakifanya jitihada za kutetea na kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto, kwani suala la kuwasaidia watoto ni la kila mmoja wetu ili kuhakikisha wote kwa pamoja wanashirikiana kutokomeza ukatili wa kijinsia ambao wamekuwa wakifanyiwa watoto kwa kiwango kikubwa.
“Kikao hiki kimeandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na sisi Shirika katika kuangalia namna ya kuweka mikakati itakayosaidia kuwaokoa watoto hawa; wapo katika hatari kubwa kutokana na ukatili wanaofanyiwa kuanzia majumbani, kwenye taasisi wanazopata huduma hali ambayo imesababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la watoto wa mitaani,” alisema Mulongo.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, ikiwemo ya Jeshi la polisi nchini Tanzania kama ilivyonukuliwa na DW, inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. katika mwaka 2020 ambapo kulikuwa na matukio 7388 yaliyoripotiwa nchini kote tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.
Ripoti hiyo ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono, ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa matukio 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015, ambapo matukio 5803 yaliripotiwa, ambayo ni sawa na matukio 615.
Hata hivyo, watetezi wa masuala ya watoto wanasema, hali ni mbaya zaidi iwapo takwimu mpya zitatolewa, kwani vitendo vya ukatili kwa watoto vimekithiri nchini kote na kila siku vyombo vya habari vinaripoti habari kuhusu vitendo hivyo, jambo ambalo linapaswa kuihamsha jamii na kukabiliana na suala hilo.