Na Subira Ally
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, amesema kwamba wakati nchi inaelekea katika mjadala wa Mageuzi makubwa ya sekta ya elimu ni wajibu kwa Wazanzibari kuwa na tafakuri ya kina juu ya umuhimu wa suala hilo na namna kulifanikisha kwake.
Othman ameyasema hayo huko hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki mjini Zanzibar, alipofungua mkutano wa pili wa kumuenzi Maalimu Seif Sharif Hamad ulioandaliwa na Maalim Seif Faoundation na kuwashirikisha wanataaluma, wanasiasa, na wanadiplomasia kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Makamu alisema, hatua hiyo ni muhimu katika jitihada za pamoja za kujenga hatma njema ya Zanzibar kielimu kwa kuzalisha vijana wenye maarifa na uwerevu wa kitaaluma hasa kwa vile Taifa imara linategemea sana kizazi makini kilichotayarishwa kukabiliana na changamoto zilizopo na zijazo.
Amefahahamisha kwamba, hali hiyo ni lazima kwenda sambamba na kuwepo maridhiano ya kweli, amani na utulivu nchini na kuwepo jitihada kubwa za kutajenga uchumi imara na kuleta maendeleo ya kweli nchini.
Aidha, Othman alisema kwamba hili hiyo ni lazima pia kuziweka katika tafakuri na tathimini sahihi rasilimali za aina mbali mbali zilizopo nchini katika kuijenga Zanzibar kuwa imara zaidi kupitia elimu itakayotolewa.
Alisema kwamba, kuwepo Zanzibar yenye uchumi imara ni muhimu katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokwamisha maendeleo ya nchi.
Othman alisema kwamba, katika kukabiliana na hali bora ya kuwatayarisha vijana kielimu ni lazima kwa serikali kutengeneza na kuwepo sera na uendeshaji bora wa sekta hiyo ya belimu unaosaidiwa na usimamizi bora sambamba na kuwepo muono sahihi katika uongozi wa ngazi mbali mbali.
Aidha, Othman alisema kumtayarisha mtoto kuwa mwerevu kielimu kutasaidiwa sana na kuwepo makuzi na malezi bora kwa kuzingatia mazingira anayoishi ikiwemo usomeshaji na kuwepo na kutumika mitaala bora huku mwalimu akipewa umuhimu wa kipekee kutokana na uwezo wake wa kumsaidia mwanafunzi kujifunza.
Othman alisema, nchi ni lazima ijitahidi kubuni mbinu tofauti zitakazosaidia kuhakikisha kwamba sekta ya elimu inazalisha vijana werevu watakaokwenda samabamba na mahitaji ya sasa na baadaye yanaongozwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa manufaa ya Taifa na kwamba jambo hilo linawezekana kufikiwa ingawa njia za kufikia zinaweza kutafautiana.
Naye Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Issa Shivji, akiwasilisha mada kuhusu uhuru wa elimu kama msingi wa Demokrasia, alisema kwamba huwezi kuwa na elimu bora bila kwepo walimu bora wanaoweza kutengeneza vipaji kwa vijana.
Alisema, walimu ndio wenye uwezo na upeo sahihi wa kukuza vipaji vya wanataaluma na kuzalisha wasomi bora wanaojiamini katika kuchangia vyema maendeleo ya Taifa lao.
Professa Shevji alisema, wanafunzi wa namna hiyo ndio wenye uwezo wa kujadili na kudadisi mawazo mbali mbali yaliyopo na kutoa mbadala yatakayosaidia vijana kuweza kuchangia upeo wa maendeleo ya nchi yao.
Nao baadhi ya washiriki katika Mkutano huo wamesema kwamba, katika kuhakikisha maendeleo bora ya elimu nimuhimu kujadili , kupanga na kuamua kuanzisha mifuko mbali mbali itakayosaida kuwa miundombinu ya kukuza maendeleo ya sekta ya elimu ili kupata vijana wenye uwezo mkubwa kitaaluma.
Mkutano huo wa Siku mbili ambao ni wa pili umetayarishwa na Maalimu Seif Foundation, na umewakutanisha wananasiasa, wataalamu, wanadiplomasia na wananchi mbali mbali utatajidili mada kadhaa ikiwa ni hatua ya kuenzi Fikra za Marehemu Maalim Seif Sharif kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwaleta wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla pamoja, kuhubiri amani na mshikamano pamoja na kuchangia ukuaji wa demokrasia na haki za binaadamu nchini.