Na Iddy Mkwama
WAKALA ya barabara Tanzania (TANROADS) imetaja mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya ujenzi kwa kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kukarabati na kuongeza mtandao wa barabara, kujenga madaraja na viwanja vya ndege kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi leo Septemba 26, 2024 jijini Dar es Salaam, kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa Vyombo mbalimbali vya habari, ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Ephata Mlavi alisema, kwasasa jumla ya Kilometa 15,343.88 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Alisema, Kilometa 1,198.50 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, Kilometa 2,031.11 zipo kwenye hatua za ujenzi kwa kiwango cha lami na Kilometa 2,052.94 na Madaraja mawili (2) yamefanyiwa upembuzi yakinifu tayari kujengwa kwa kiwango cha Lami.
“Jumla ya Kilometa 4,734.43 na Madaraja 10 yapo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu. Miradi ya Barabara yenye urefu wa Kilometa 5,326.90 na Madaraja saba (7) ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami,” alisema.
Mbali na barabara hizo, Mhandisi Mlavi alisema, madaraja tisa yamejengwa ambayo ni Gerezani – Dar es Salaam, Tanzanite – Dar es Salaam, Wami – Pwani, Kitengule – Kagera, Kiyegeya – Morogoro, Ruaha – Morogoro, Ruhuhu – Ruvuma, Mpwapwa – Dodoma, Msingi – Singida.
Pia, madaraja mengine yapo kwenye hatua za utekelezaji likiwemo la Pangani – Tanga, J.P. Magufuli – Mwanza, Lower Mpiji – Dar es Salaam, Mbambe – Pwani na Simiyu – Mwanza, huku wakitarajia kujenga madaraja mengine kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mhandisi Mlavi alitaja madaraja hayo kuwa ni Godegode, Mtera – Dodoma, Ugala – Katavi, Kamshango, Kyabakoba, na Kalebe – Kagera, Bujonde, Bulome, Ipyana – Mbeya, Chakwale, Nguyami, Mkundi, Mjonga, Doma, Mkondoa – Morogoro, Lower Malagarasi – Kigoma, Sanga – Songwe, Kilambo – Mtwara na Chemchem – Singida.
“Pia, katika Ilani ya Chama, Daraja la Jangwani limesanifiwa na Mkataba wake wa Ujenzi utasainiwa hivi karibu kabla ya Mwezi Agosti 2024 kuisha,” alisema.
Kwa upande wa viwanja vya ndege alisema, tayari viwanja saba vimekamilika ambavyo ni Julius Nyerere (Terminal Three), Mwanza, Mtwara, Songea, Songwe (Runway), Songwe (Supply and Installation of Airfield Ground Lights (AGL) na Geita. “Miradi nane inaendelea ambayo ni Msalato, Iringa, Musoma, Tabora, Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma na Moshi.”
Katika hatua nyingine, Mhandisi Mlavi kwenye mkutano huo na wahariri alisema, TANROADS imepokea fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kusimika taa za barabarani nchini kote.
“Mikoa ambayo tayari imekwisha simikwa taa hizo kwenye baadhi ya Barabara zake ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimajaro, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Songwe, Tabora, Tanga,” alisema.
Aidha, alisema mbali na ujenzi wa barabara, madaraja na viwanja vya ndege, Wakala imefanya kazi kubwa katika kurejesha hali ya miundombinu baada ya kukumbwa na adha ya Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.
Alisema, pamoja na shughuli hizo za ujenzi wanazozifanya, pia wanaendelea na jitihada za kuwajengea uwezo Makandarasi Wazawa ambapo kila mwaka wanatenga asilimia kumi (10%) ya bajeti kwa ajili ya Miradi ya mafunzo kwa vitendo, huku wakipanga kutenga asilimia thelathini (30%) ya bajeti ya maendeleo kwa ajili ya upendeleo kwa wazawa na kutenga asilimia tano (5%) ya bajeti ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya makundi maalum.
“Kazi za matengenezo ya barabara na madaraja zitekelezwe na Makandarasi Wazawa na kusimamiwa na Washauri Elekezi Wazawa tu,” alisisitiza, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Ephata Mlavi.