Na Linus Siwiti
AJALI za barabarani zimekuwa gumzo kuanzia mwanzoni wa mwaka 2023 hadi mwisho, ambapo kila kukicha tumesikia taarifa zinazotolewa kuhusiana na tatizo hilo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza maisha ya watu na kusababisha wengine kuwa walemavu wa muda au wa kudumu.
Tunashuhudia matukio hayo yakihusisha kila aina ya chombo; magari madogo, makubwa, pikipiki, magari binafsi na yale yanayobeba abiria. Kwa mfano hivi karibuni ajali iliyotikisa zaidi ni ile ya kichwa cha treni kugongana na basi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 13.
Huo ni mfano mmoja tu wa ajali mbaya zilizotokea mwaka 2023, ila zipo nyingi na zimetokea kwenye maeneo tofauti tofauti na kusababisha pigo kwa Taifa, familia na ndugu wa karibu wa marehemu waliopoteza maisha au kujeruhiwa vibaya.
Tutambue kuwa, kila palipo na tatizo basi kuna chanzo cha tatizo hilo; zipo sababu nyingi zinazotolewa baada ya kutokea ajali ambapo utasikia ikielezwa chanzo ni uzembe wa madereva, mwendokasi na ubovu wa chombo kilichopata ajali au kusababisha ajali.
Kwamba, wahusika wameshindwa kufanyia vyombo vyao matengenezo ya mara kwa mara (service), au utasikia wengine wanasema ni ukosefu wa umakini wa dereva.
Kwa upande wangu nakubaliana na sababu hizo zinazotajwa kila mara na kubwa ni suala la mwendo kasi wa vyombo vya moto na uzembe wa baadhi ya madereva ambao wanasababisha ajali barabarani.
Ukifika kwenye eneo ambalo limetokea ajali, ukiwauliza mashuhuda ni lazima watakuambia kuhusu suala la mwendo kasi, maana ni moja ya vyanzo vya ajali; na jambo baya zaidi hata baadhi ya abiria wamekuwa wakiwafurahia madereva wanaoendesha kwa mwendo kasi.
Ndio maana, sio ajabu ukiwa kwenye magari ya aina hiyo ukasikia “Safi Safi dereva, ongeza ongeza mwendo, koleza baba koleza,” haya utayashuhudia zaidi kwenye vyombo vya usafiri ambavyo vimekodiwa kwa ajili ya matukio fulani kama vile harusi nk. Hatupaswi kuwa wapole na kufurahia na kunyamaza pale dereva anapokuwa katika mwendo hatarishi.
Jeshi la Polisi hususani kitengo cha Usalama Barabarani wasichoke kutoa elimu kwa raia wake na madereva kuhusu usalama wao, vyombo wanavyoendesha na abiria wanaowabeba na hata watembea kwa miguu. Ukiachilia mbali mwendokasi na ubovu wa chombo cha moto cha usafiri; tatizo jingine kubwa lipo kwa madereva wenyewe.
Hapa kuna haja ya kuwekwa mkazo Elimu ya Saikolojia ambayo ndio itadhibiti ongezeko la ajali za barabarani; Jeshi la Polisi linapaswa kufanya kampeni kubwa na kutoa elimu kwa kushirikiana na watalaamu wa Saikolojia kushughulikia baadhi ya maeneo.
Kwanza, Msongo wa mawazo. Kwa mujibu wa watalaamu wa masuala ya afya, huu ugonjwa mbaya ambao unamfanya mtu akose utulivu wa akili na apoteze umakini katika kuamua na kufanya mambo katika hali ya usahihi na uzingativu wa viwango vya juu.
Dereva ambaye anaendesha chombo cha moto akiwa na tatizo hili, uwezekano wa kusababisha ajali ni mkubwa, hivyo elimu ya kuwaondoa kwenye hali hiyo itawasaidia madereva.
Aidha, hatua ya awali ambayo dereva anapaswa kuichukua iwapo atagundua ana msongo wa mawazo ni kuachana kuendesha chombo cha moto, kisha awatafute watalaamu wa kada ya afya na Saikolojia ili apate tiba ya kuondokana na ugonjwa huu.
Pili; Hali ya uthibiti hisia, (avoiding over emotional fillings). Hisia sio mbaya ila haipaswi kupitiliza. Mfano;- wakati madereva wanaendesha inawezekana ikawa gari au pikipiki kuna hali fulani inaweza kuingia ndani, na kujikuta anaendesha mwendo mkali na pengine anajihisi kupata raha na kuifurahi safari, dereva anaweza asione shida yoyote, ila hilo ni tatizo kubwa linalohitaji elimu ya kudhibiti hisia. Katika eneo hili inatakiwa kuwasaidia kwa kiwango fulani kujizuia japo sio jambo jepesi.
Tatu, Saikolojia ya kuondokana na hali ya uraibu wa matumizi ya vileo; matumizi ya vileo kwa madereva na hata ambao sio madereva athari zake ni kubwa, vileo kama pombe, mirungi, bangi na vinavyo fanana na hivyo ni miongoni mwa vyanzo vinavyosababisha ajali, kwani vinaondoa hali ya akili ya kawaida, na kupoteza umakini wa hali ya juu barabarani.
Uwepo wa elimu ya Saikolojia kwa ajili ya kuondokana na uraibu wa matumizi ya vileo itasaidia kuthibiti ajali, tena kama ikiwezekana, Jeshi la Polisi Usalama barabarani, kama lilivyofanikiwa kuweka vifaa vya uthibiti mwendo kasi hali maarufu kama ‘Tochi’ barabarani, ni vema wakaweka utaratibu kwa madereva kupimwa viwango vya matumizi ya vileo (alcoholic PH).
Hata hivyo, mbali na elimu ya Saikolojia, Sheria kali kwa ajili ya kuwabana madereva wanaotumia vileo wakati wanaendesha vyombo vya moto zinapaswa kuwepo. Naamini hakuna dereva ambaye atakubali aingie matatani kwa kuendesha chombo cha moto akiwa ametumia kileo cha ina yoyote.
Ushauri wangu ni kwamba, kila mwananchi ana wajibu wa kulinda usalama wake binafsi na usalama wa watu wengine mali za umma na binafsi; abiria wanapaswa kutofumbia macho hali ya mwendo kasi wa madereva.
Pia, madereva wakubali kupokea elimu na ushauri mbalimbali na kufanyia kazi, wasipitwe wasipitwe na mafunzo ya udereva, elimu kutoka Jeshi la usalama barabarani kuhusu kuzingatia kanuni na Sheria yanayotolewa kila mara. Nilinde nikulinde sote kwa pamoja tukilindana, uthibiti wa ajali barabarani inawezekana!
*Mwandishi wa makala ni Mwalimu kitaaluma, ni mshauri na mhamasishaji, pia ni mwandishi wa kitabu cha ‘IJUE NJIA ILIYO SAHIHI.’ Kwa maoni na ushauri +255(0)0785759909.