JESHI la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano ambayo yametangazwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 23, jijini Dar es Salaam.
Mbowe alitangaza maandamano hayo, kwenye Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni, wakati akitoa msimamo wa chama hicho kufuatia matukio ya utekaji yanayoendelea nchini.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema, iwapo Serikali haitawarudisha viongozi wao waliotekwa, sambamba na kuwatangaza wahusika wa vitendo hivyo vya utekaji, wataandamana kuanzia Septemba 23, 2024.
Akitangaza kupiga marufuku maandamano hayo leo Septemba 13, 2024 Mkoani Kilimanjaro, Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP David Misime alisema, anashangazwa na kitendo cha viongozi wa chama hicho kuitisha maandamano wakati uchunguzi wa matukio hayo unaendelea.
Aidha, tayari Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi hilo na vyombo vingine vya Usalama kufuatilia na kuwasilisha taarifa.
“Tunajiuliza na tunaendelea kufuatilia, kwanini wanataka kututoa kwenye reli ya hatua za kiupelelezi zinazoendelea baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuvielekeza au kuviagiza vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kisha wawasilishe taarifa kwake,” alisema Misime.
Misime alisema, imekuwa ni kawaida kwa viongozi na wafuasi wa Chadema, kupanga na kuratibu mipango kadhaa na kutoa matamshi yenye lengo la kutaka vurugu nchini, ili kuharibu amani ya nchi kwasababu wanazozijua wenyewe.
“Tunatoa onyo kwa viongozi wa chama hicho kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha katika uhalifu huo. Yeyote atakayeingia barabarani, atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi, kwa maana hiyo, maandamano hayo yamepigwa marufuku,” alisema.
Aliongeza: “Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam, kutoka Mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo, asithubutu kufanya hivyo, kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika, hivyo asipoteze muda na gharama zake.”
Misime alitoa rai kwa wananchi wapenda amani kutokubali kurubuniwa, kudanganywa au kushawishiwa kwa namna yoyote ile kushiriki katika maandamano hayo, badala yake waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Hata hivyo, sio mara ya kwanza kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya maandamano yaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi, jambo ambalo limekuwa likisababisha vifo, majeruhi na hasara ya mali za watu kwenye maeneo yanapofanyika maandamano hayo.
Itakumbukwa, mwaka 2010 viongozi wa Chadema waliwachochea wafuasi wao kwenda kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha kwa lengo la kuwatoa kwa nguvu wenzao waliokamatwa kwenye maandamano yaliyopigwa marufuku.
Kutokana na agizo hilo la viongozi, kulizuka vurugu kubwa ambazo zilisababisha vifo vya watu watatu vilivyotokana na mapambano makali kati ya raia na askari.
Mbali na tukio hilo, mjini Morogoro kijana Ali Zona alipoteza maisha wakati wa maandamano yaliyohamasishwa na viongozi wa Chadema, na mwaka 2018, jijini Dar es Salaam, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwilini alipoteza maisha kwenye maandamano ya chama hicho.
Kwenye maandamano hayo yaliyoanzia kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, mbali na kifo cha mwanafunzi huyo, wafuasi wengine wa Chadema na wapita njia walipata majeraha, huku wafuasi 28 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Ili tusirudie yale yaliyojitokeza miaka ya nyuma ambapo watu walipoteza maisha kwenye maandamano kama haya, nashauri viongozi wa Chadema watafute njia za kistaarabu za kumaliza mivutano yao na vyombo vya dola ikizingatiwa tayari walianza maridhiano na Serikali,” alisema Mohamedi Mustafa, mkazi wa Ilala.
Alisema, sio jambo la busara kushindana na vyombo vya dola ambavyo vipo kwenye kazi ngumu ya kuhakikisha wanachunguza na kudhibiti matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea hivi sasa.
“Tuviache vyombo vya dola vifanye kazi yake, ni dhahiri maandamano haya zaidi ya kusababisha madhara kwa watu, hayatatupa majibu ya giza ambalo limetanda hivisasa hapa nchini kwetu,” alisema na kuwasihi watanzania hususani wa jiji la Dar es Salaam, kujiepusha na maandamano hayo ambayo yamepigwa marufuku.