Maafisa bajeti watakiwa kuzingatia maadili na weledi

0

Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI

MKURUGENZI wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Angelista Kihaga, amewataka Maafisa Bajeti wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, uadilifu na weledi ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo.

Akizungumza leo Septemba 9, 2025 kwenye mafunzo ya uandaaji wa mipango na bajeti kwa Maafisa Bajeti wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri yanayoendelea katika Chuo cha Mipango Jijini Dodoma, Kihaga amesema wajibu wa maafisa hao ni kuhakikisha rasilimali za umma zinapangwa na kutumika kwa tija, kwa manufaa ya wananchi.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha mnazingatia maadili ya kazi na kufanya kila jambo kwa weledi. Taifa linawategemea katika kuhakikisha bajeti mnazoandaa zinagusa mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Kihaga.

Aidha, amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza ufanisi katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti, huku akiwataka washiriki kutumia fursa hiyo kujifunza kwa bidii na kubadilishana uzoefu.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na maafisa bajeti zaidi ya 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Hili ni kundi la tatu kushiriki mafunzo hayo, ambapo kesho inatarajiwa kuanza kundi la nne.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here