Lipi vazi rasmi la Tanzania kwasasa?

0

Na Mohamed Kazingumbe

MAMA Salma Kikwete, ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Ni mama asiye sahaulika kwa urithi wake kwa Taifa la Tanzania katika nyanja mbali mbali za kiutamaduni.

Ni mwana-mama aliyejitokeza bila kupiga baragumu kwa wananchi wa taifa la Tanzania juu ya falsafa yake ya kujikobeka upande wa kitenge au kanga au mgolole begani sambamba na suti yake safi. Ni katika kipindi chote cha utawala wa mumewe, aliyejulikana kwa herufi mbili,” JK” (2005 – 2015).

Bila kutambua kuwa wananchi kumbe wamekuwa mstari wa mbele katika kutazama mavazi ya viongozi ili waige aina nzuri ya kivazi. Mama Kikwete amewavutia wanawake lukuki katika mtoko wa kubeba upande wa khanga au kitenge begani katika nyakati za tafrija au hafla, matamasha na dhifa za kitaifa.

Kivazi hiki kimeonekana kuwapendeza wengi hali ambayo imekuja kuleta mjadala kwa dhana kwamba, wengi hususani kwa upande wa akina-mama kupendezewa na mtoko huo; na kufaa ungekuwa ni mtoko rasmi kwa wanamama kitaifa.

Tuje katika dhana yote ya ubunifu wake; ni historia ya kuigwa katika nchi hii hususani katika upande wa wanawake, kwani hapana ubishi pambo hilo limekuwa linawaweka unadhifu mkubwa usomi mwa jamii. Sina uhakika kama ubunifu wake umekuwa unalenga kiitikadi, lakini matunda yake ni kwa wanawake wote wa imani zote, naamini hivyo.

Haijafahamika vizuri kama ubunifu wake aliupata wapi, lakini tumeshuhudia kipindi kizuri kwa wanawake wakining’iniza khanga au kitenge begani na kuleta sura inayowatambulisha akina mama wanapotembelea ng’ambo.

Historia inabainisha kwamba, moja ya silaha ya mila au desturi – utamaduni wa taifa Fulani, ni pamoja na mavazi na uvaaji wake.

Mapema wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanzania, viongozi wa ngazi ya kitaifa, hususani wanasiasa- kivazi chao kilionekana cha kujifunga lubega. Hali hiyo ilitambulisha wenye kivazi kile ni wanasiasa.

“Wewe umevaa vazi kama anavyovaa Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Oscar Kambona,” Mzee mmoja alisema alipoulizwa juu ya ubunifu wa Mama Kikwete dhidi ya kivazi hicho katika historia ya nchi hii.

Haikufahamika kifasaha wapi Nyerere wenzake walipata kivazi hicho cha mgolole, lakini wadadisi wa kisiasa wanafikiri kwamba Nyerere alipata kuleta uvaaji huo kutoka katika baadhi ya makabila nchini Tanzania au kwa wanasiasa wenzake wakongwe kama vile Kwame Nkrumah wa Ghana.

Dhana hiyo inakuja kutokana na ukweli kuwa, Kwame Nkrumah aliipatia nchi yake uhuru kutoka kwa wakoloni mwaka 1957; kipindi hicho Nyerere akiwa na miaka mitatu tu tangu aanzishe TANU (Tanganyika African National Union).

Hali ya kutafuta vazi maalumu la kitaifa limeletwa usoni mwa watanzania mara kadhaa bila mafanikio. Vazi la “Chou En Lai” lilitawala kipindi kirefu baada ya Serikali ya Nyerere kuiga vazi la Waziri Mkuu wa China aliyetembelea nchi hii mapema baada ya Tanganyika kupata uhuru. Raha pia ikazidi kunoga baada ya muungano wa mataifa haya mawili Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964.

Mwalimu Nyerere na Shehe Amani Abeid Karume kivazi chao wakati wote ni ‘kata shingo’ yaani Chou En Lai’, vazi ambalo hadi leo wanasiasa wa enzi za Nyerere kama vile, John Malecela au Job Lusinde bado wana kumbukumbu ya vazi hilo.

Ni kama haitoshi likaja vazi la “Kaunda” na “Ngwabi” mavazi hayo mawili ambayo yalikuja kuwavutia watanzania. Ni mvao wa rais wa kwanza na Zambia aliyekuwa rafiki mkubwa wa Nyerere.

Na mtindo wa “Ngwabi”, ni vazi lililotumika na Rais wa Jamhuri ya Kongo Brazaville. Lakini mitindo yote hiyo ilikuja kufifia na Tanzania, ikawa haina mtindo maalum wa kitaifa. Maana yake haijulikani hadi leo, hakuna jibu.

Mama Kikwete mbali ya kuleta mtindo wake huo, hakuishia hapo alikuja na falsafa, ya “Mtoto wa mwenzio ni wako, na sio mkubwa mwenzio”. Ni kauli inayowakumbusha jamii kuwa wamoja na kuwajibika katika utunzaji wa maadili mema kwa watoto wetu.

Huo ni utamaduni wa asili. Enzi za leo hakuna anayeweza kumkanya mtoto wa mwenzake, hali ambayo imechangia kuvurugika utamaduni, mila na desturi tuliyoachiwa na wahenga.

Haijafahamika kiundani juu ya ubunifu huo wa kivazi cha kukobeka upande wa kitenge katika bega la kushoto aliupata wapi? Lakini wamama kwa wadada waliinukia kuenzi mtindo huo kiasi kwamba hata wanawake wa nchi jirani nao waliinukia kuupenda na kuiga kupeleka kwao, hususani wale wa kanda ya Afrika ya kati na mashariki.

Ubunifu wake haukuachwa bila kufanyiwa kazi na Gazeti hili. Huku tukiwa katika kutafakari kama tutakuja kupata vazi au mtindo maalumu wa kitaifa ni lazima ufanyike uamuzi wa makusudi lipatikane vazi la taifa la Tanzania kwa jinsi zote.

Mara kadhaa wana mitindo wamekuwa majaribuni kusubiri watakuja na vazi gani! Kigugumizi katika wizara ya utamaduni juu ya maamuzi ni kizungumkuti. Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, ilikuja kuporomosha suala la vazi maalumu la kitaifa au lile mahususi kwa viongozi wa kitaifa wakaonekana kurejea kule tulikotoka kwa wakoloni.

Hivi sasa mambo ni magumu zaidi kwani viongozi wa Kitaifa ni suti mbele kwa mbele. Magari makubwa makubwa meusi, nadhani itakuwa ni kauli mbiu ya taifa kwamba Watanzania ni watu wa suti, tai ndani ya magari meusi. Hivyo ndivyo ninavyoamini mimi, naomba kuwakilisha.

0715687454

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here