Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri, madereva na abiria kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua kubwa, kwa kuzingatia taarifa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Wito huo umetolewa leo Septemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habib Suluo wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH).
Dkt. Suluo amesema, usalama wa abiria na mali zao unapaswa kupewa kipaumbele, hasa katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko, maji yanayotiririka kwa kasi na uharibifu wa miundombinu.
Amewataka wamiliki na madereva kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri kabla ya kuanza safari, akitaja umuhimu wa kukagua matairi, mfumo wa breki, vioo, mfumo wa kufuta maji kwenye kioo (wipers) pamoja na taa za magari.
Vilevile, amesisitiza kuwa ukaguzi huo ni muhimu zaidi wakati wa mvua, kwa kuwa hali ya hewa inaweza kupunguza muonekano wa dereva na kuongeza changamoto katika uendeshaji wa magari.
Dkt.Suluo pia amewataka madereva kuepuka kujaribu kuvuka maeneo yenye maji yanayotiririka kwa kasi au madaraja yaliyofunikwa na maji.
Amesema, kabla ya kuvuka maeneo hayo, dereva anapaswa kuhakikisha kina cha maji na uimara wa daraja viko salama, akieleza kuwa katika baadhi ya mazingira maji yanaweza kuwa yamesababisha mmomonyoko wa udongo chini ya miundombinu bila kuonekana kwa urahisi.
Kwa upande wa usafiri wa reli, LATRA imezitaka kampuni na wasimamizi wa reli kufanya ukaguzi wa kina wa njia za treni, ikiwamo reli za zamani za meter gauge ili kuhakikisha kingo za reli na udongo unaozunguka njia hizo vina uimara unaohitajika.
Mkurugenzi Mkuu amesema, ukaguzi huo unapaswa kuzingatia hali ya njia kabla na baada ya mvua kubwa ili kupunguza uwezekano wa madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mmomonyoko wa udongo au kuharibika kwa miundombinu ya reli.
LATRA pia imewasihi wananchi kupanga safari zao kwa kuzingatia hali ya hewa na kuahirisha safari zisizo za lazima pale kunapokuwa na mvua kubwa au mazingira hatarishi.
Aidha, wazazi na walezi wanaosafiri na watoto wametakiwa kutumia programu ya LATRA App kufuatilia usalama na mwenendo wa magari wanayosafiria, hususan katika safari za kati ya miji.
Dkt. Suluo amesema, magari ya abiria yana mifumo ya ufuatiliaji inayowezesha kufuatwa kwa mwenendo wa safari, hivyo abiria wanaweza kutumia teknolojia hiyo katika kupata taarifa zinazohusiana na safari zao.
LATRA imeeleza pia kuwa mfumo wake wa huduma kwa wateja utaendelea kupatikana saa 24 kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, kutoa msaada na kufuatilia masuala ya usalama wa usafiri nchini.