Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo (WMA) Mkoani Dodoma umewataka wauzaji wa gesi ya majumbani wakiwemo mawakala wa bidhaa hiyo kuzingatia sheria na miongozo ya vipimo.
Mawakala hao wametakiwa kuwa na mizani iliyohakikiwa pamoja na kuhakikisha mitungi ya gesi inapimwa kabla ya kuwauzia wananchi ili kuhakikisha wanapata kiwango sahihi cha gesi wanacholipia.
Hayo yamesemwa na Meneja wa WMA Mkoani Dodoma Said Ibrahim wakati wa zoezi la ukaguzi kwa mawakala na wauzaji wa mitungi ya gesi, ambapo ukaguzi huo unalenga kulinda haki za walaji pamoja na kuhakiki usahihi wa vipimo vya bidhaa hiyo.
Alisema, wafanyabiashara wanaouza gesi ya majumbani bila kuwa na mizani, wanafanya kosa na endapo watabainika, watachukuliwa hatua kali za kisheria kama wakosaji wengine.
“Nawasihi kuwa na mizani ya kupimia gesi, kutokuwa na mizani ya kupimia gesi kwenye duka lako la kuuzia gesi ni kosa kwa mujibu wa sheria ya vipimo, pia ni kosa la jinai,” alisema Ibrahim.