Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, amesema kuendelea kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) Zanzibar ni hatua muhimu katika kulinda amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Abdi amesema hayo akiwa Jimbo la Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea matawi ya CCM kwa ajili ya kukagua uhai wa chama na kusikiliza changamoto za wanachama.
Akizungumzia kuapishwa kwa Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Abdi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa na vyama vya CCM na ACT-Wazalendo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Othman Masoud aliapishwa Septemba 22, 2026, katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar, ikiwa ni hatua katika utekelezaji wa maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT-Wazalendo.
Abdi amesema Zanzibar imepitia vipindi ambavyo tofauti za kisiasa zilikuwa zikisababisha migawanyiko katika jamii, hasa baada ya uchaguzi, hali iliyowafanya wananchi kutengana kwa misingi ya vyama vya siasa.
“iliwahi fika wakati Zanzibar ilikuwa kila baada ya uchaguzi watu wanapigana, tunasusiana, hawaendi kuzikana, hawashirikiani. ilikuwa maneno mengi na malumbano,” amesema.
Amesema hatua ya kuapishwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za kujenga maridhiano na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa Zanzibar.
Ameeleza kuwa jambo la msingi kwa wananchi ni kuhakikisha tofauti za vyama haziwi chanzo cha kuvunja mshikamano wa jamii, huku kila chama kikiendelea na shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
“Wito wangu kwa wanasiasa wenzangu ni tushirikiane katika jamii, lakini pia kila mtu ana chama chake cha siasa,” amesema.
Aidha, Abdi amesema CCM itaendelea na shughuli zake za kisiasa na kuimarisha chama, huku akisisitiza kuwa ushirikiano katika jamii unapaswa kupewa nafasi bila kujali tofauti za kisiasa.
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema maridhiano hayo yanalenga kuimarisha amani, umoja na utulivu, huku nguvu zikielekezwa katika maendeleo na kushughulikia changamoto za wananchi.