HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inaendelea na kambi maalum ya upasuaji wa upandikizaji wa meno bandia kwa njia ya kisasa ambayo inafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 10 hadi 14, 2024.
Kambi hiyo inayofanywa na wataalam wa ndani kwa kushirikiana na Daktari Bingwa aliyebobea katika upasuaji wa taya kutoka Hospitali za Wochhardt Dkt. Chirag Desai ambapo kwa kipindi hiki cha siku tano wanatarajia kufanya upandikizaji kwa wagonjwa 30.
Upandikizaji huu wa meno bandia utahusisha kupandikiza jino la mgonjwa moja kwa moja kwenye mfupa wa taya yake na kulifanya jino hilo kujishikiza moja kwa moja kama jino la kawaida hivyo haliwezi kutoka kama yalivyo meno mengine ya bandia.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Kinywa na Meno, Dkt. Agrey Shao mwitiko wa watu kufanya upasuaji wa kupandikiza meno bandia umekuwa mkubwa ambapo hapo awali walilenga kupandikiza wagonjwa 20 na hivyo idadi ya wanaopandikizwa imezidi malengo waliojiwekea kulingana na mahitaji ya walio wengi.
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeendelea kufanya matibabu ya ubingwa bobezi ambayo yamesaidia kupunguza rufaa na usumbufu wa Watanzania kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu hayo ambayo yanagharimu kiasi kikubwa cha fedha.