Jussa avurugwa na kasi ya kuongezeka kwa hoteli kubwa za Kitalii Z’bar

0

WAKATI Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Ismail Jussa wakiendelea kufanya propaganda kwa lengo la kuuaminisha umma kwamba, SMZ imeshindwa kutengeneza mazingira ya kuinua uchumi wa nchi hiyo na kuongeza ajira, hali imekuwa tofauti.

Kuongezeka kwa hoteli kubwa za kitalii, kunatajwa kuchochea kuongezeka ukuaji uchumi wa Z’bar, jambo ambalo linakwenda kinyume na kauli za chama hicho na inaelezwa suala hilo linamuumiza kichwa Jussa na chama chake.

Chama hicho kupitia kwa Jussa, kimekuwa kikitoa kauli zenye lengo la kutaka kuonyesha kwamba, uwekezaji unaofanyika visiwani humo hauna tija kwa nchi na wananchi na nchi hiyo, lakini takwimu zinaonyesha mwelekeo mzuri.

Wananchi waliozungumza na Mwandishi Wetu visiwani humo wamesema, wanaridhishwa na jitihada zinazofanya na SMZ chini ya Dkt. Hussein Mwinyi, hususani kwa kutengeneza mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji wanaojenga hoteli kubwa za Kitalii.

“Tunaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Rais wetu Dkt. Mwinyi kuwavutia wawekezaji, wanapokuja na kujenga hoteli kubwa, tunapata ajira, uchumi wa nchi yetu unakua, tunamuomba asisikilize maneno ya akina Jussa, aendelee kutupigania wananchi wake,” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Masudi, ambaye anajihusisha na masuala ya utalii.

Mapema leo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka Mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili kuongeza Idadi ya wawekezaji kwa kuimarisha huduma ikiwemo Ujenzi wa Viwanja vya Ndege, Barabara, Miundombinu ya Maji, Umeme na Afya.

Rais Dkt.Mwinyi alisema hayo baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Hoteli ya SANDIES NUNGWI BEACH RESORT ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameziagiza Taasisi, wadau na wananchi kuendelea kushajihisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili Zanzibar inufaike zaidi na Mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, Uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia 7.5 kunakochangiwa kwa kiasi kikubwa na Sekta ya Utalii.

Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi amezitaja faida kuu za uwekezaji hapa nchini kuwa ni ukuaji wa Uchumi, ongezeko la Watalii, ongezeko la Kodi na upatikanaji wa fursa za ajira hususani kwa Vijana.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Mamlaka ya Uwekezaji ya Zanzibar (ZIPA) kwa kupunguza Muda wa Upatikanaji wa vibali vya Uwekezaji.

Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa wawekezaji wote kuhakikisha miradi yao inawanufaisha wananchi kwa kuondoa matatizo yaliyomo ndani ya jamii ikwemo ukosefu wa huduma za Maji Afya, meme na Elimu.

Hoteli ya Sandies Nungwi Beach Resort inayomilikiwa na Kampuni ya Away Hotels Zanzibar Limited kwa asilimia 99 na Paolo Ross raia wa Italia kwa asilimia, itagharimu Dolla Milioni 17 hadi kukamilika kwake ina vyumba 126 na kutoa fursa za ajira 200.

Wakati huo huo, wachambuzi wa masuala ya uchumi wamesema, wanaamini kuongezeka kwa wawekezaji visiwani humo, ni kutokana na sera nzuri za uwekezaji za Z’bar na mazingira mazuri ya uwekezaji.

“Kama mazingira ya uwekezaji yasingekuwa mazuri na sera za uwekezaji zingekuwa mbaya kama tunavyosikia wanavyosema wanasiasa wa upinzani, wawekezaji wasingekuja kwa wingi Z’bar, lakini naamini wanavutiwa na uongozi wa Rais Mwinyi,” alisema Joseph Simon.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here