Jinsi Madini yalivyogeuka janga nchini Ghana

0

Na Charles Charles

SHERIA ya Madini ya Mwaka 1986 iliweka mfumo rasmi wa kisera kuhusu uchimbaji wa madini nchini Ghana. Ulijumuisha pamoja na mambo mengine, utaratibu mzima wa kisheria wa kulipa kodi na mirabaha mbalimbali kutokana na sekta hiyo.

Pamoja na kuonekana kukidhi malengo, lakini sheria hiyo bado ilikuja ikafanyiwa marekebisho kadhaa ya msingi ilipofika mwaka 1994, kisha ikaingizwa kwenye Katiba ya nchi hiyo ilipopita miaka sita baadaye ili iweze kuwa na nguvu pamoja na kufanya kazi zaidi.

Hata hivyo, marekebisho hayo (amendments) yalilenga zaidi katika kufanya marejeo ya msingi kwa maeneo ya ushuru, kodi, malipo ya mirabaha na kuweka muda maalum wa matumizi ya leseni za madini za wachimbaji na wafanyabiashara katika sekta hiyo.

Kana kwamba haitoshi, sheria mpya tatu zaidi zilitengenezwa baada ya sekta hiyo hiyo kuanza kuwatambua rasmi wachimbaji wadogowadogo, hali iliyokuwa tofauti kabisa na mwanzo.

Ilianzishwa Sheria ya Zebaki, Sheria ya Shirika la Masoko ya Madini na Sheria ya Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu iliyokuwa ikisimamia usajili, utoaji wa leseni na kuanzisha pia vituo ambavyo jukumu lake kubwa ilikuwa kuwawezesha kwa kuwakopesha fedha kwa ajili ya kufanyia mitaji.

Sheria ya Zebaki ilihalalisha ununuzi, usambazaji na biashara ya madini hayo ambapo, Sheria ya Shirika la Madini ilikuwa ikihusu utambuzi wa soko rasmi la huduma ya uchimbaji na biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo hasa wa dhahabu na almasi katika upande wa kwanza, na pia ilijikita kusaidia biashara ya madini hayo yenyewe, chuma na bidhaa za mapambo yaliyotengenezwa kwa madini zinazosafirishwa kwenda nje ya Ghana katika upande wa pili.

Lakini, ili sheria hizo zifanye kazi kwa uhakika ziliwekwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mamlaka mbili, kila moja ikipewa majukumu yake ambazo ni Wizara ya Ardhi na Maliasili pamoja na Kamisheni ya Madini.

Katika kufanya hivyo, Wizara ya Ardhi na Maliasili ndiyo inahusika na shughuli zote za usimamizi na utafiti wa madini, na pia ndiyo inayotengeneza sera na kuzisimamia.

Aidha, Kamisheni ya Madini iliyoanzishwa chini ya Sheria Na. 269 ya Mwaka 1992 ya Katiba ya Ghana na Sheria ya Kamisheni ya Madini ya Mwaka 1986, ndiyo taasisi kuu inayotengeneza na kusimamia mfumo mzima wa shughuli zote zinazohusu sekta ya madini.

Inasimamia Sheria ya Madini, kuhuisha Sera ya Madini, kutangaza biashara ya madini katika soko la ndani na kuishauri serikali mambo yote yanayohusika katika sekta hiyo.

Hata hivyo, taasisi hizo zote zinatekeleza majukumu yake pia kwa kusaidiwa na wakala mbalimbali kama Wakala wa Kutunza Mazingira, Idara ya Upimaji wa Ramani za Maeneo Yenye Madini, Idara ya Madini, Kamisheni ya Ardhi na Kitengo cha Madini.

Wakala wa Kutunza Mazingira (Environmental Protection Agency) au EPA ulioanzishwa kwa Sheria ya Wakala wa Kutunza Mazingira ya Mwaka 1994, unahusika na majukumu ya shughuli zote zinazohusu hifadhi ya mazingira nchini humo.

Mbali na hayo, ofisi hiyo ina jukumu la kutengeneza na kuhuisha sera, kuratibu na kufanya marekebisho mbalimbali ya sheria na taratibu zinazohusu mazingira.

Kitengo cha Madini ndani ya EPA katika upande wake kina jukumu la kuandaa taratibu za msingi kuhusu sekta ya madini, moja kati yake ikiwa ni kuratibu, kuandaa pamoja na kutoa leseni zinazohusu mazingira baada ya kujiridhisha kwamba hakuna athari za kimazingira katika miradi inayoombewa vibali hivyo.

Kina jukumu la kuratibu pia shughuli zote zinazohusu madini, kufanya tathmini ya mazingira katika maeneo ya migodi, kupokea na kufanyia utafiti na ufuatiliaji kwa malalamiko yoyote yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli zote zinazohusiana na uchimbaji wa madini na kuweka mikakati ya kutunza mazingira sehemu hizo.

Katika upande wake, Idara ya Upimaji wa Ramani za Maeneo Yenye Madini ina jukumu la kufanya utafiti wa kuzuia uchafuzi wa mazingira migodini, kisha inaishauri serikali juu njia bora zaidi za kufanya ili kufanikisha jambo hilo. Lakini, ya licha ya kuwa na sera na taasisi hizo zote, maeneo ya migodi bado ni tatizo na kitisho kikubwa dhidi ya mazingira nchini Ghana.

Miongoni mwa mambo yanayosababisha uharibifu wa mazingira ni mapungufu katika uratibu wa taasisi husika, udhaifu wa uongozi wa shughuli za madini na hasa aina ya zebaki, kutoshirikishwa kikamilifu kwa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi katika ulinzi na hifadhi ya mazingira, mlolongo mpana wa usajili wa wachimbaji wadogo na elimu duni ya utunzaji wa mazingira waliyonayo wananchi.

Aidha, shughuli za madini nchini humo pia zimeharibu miundombinu ya vyanzo vya maji, kuathiri uoto wa asili, kuharibu ardhi ama kupotea kwa rutuba iliyokuwa katika maeneo yanayofaa kwa kilimo kabla ya kuvamiwa na wachimbaji wa madini.

Mbali na hayo, kampuni ya Bilington Bogoso Gold ambayo sasa inaitwa Golden Star Resources Bogoso/Prestea Limited ilifanya uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo hilo la Prestea.

Katika kufanya hivyo, kampuni hiyo ilijenga bwawa la kutitirishia maji yenye sumu zitokanazo na usafishaji wa madini yaliyokuwa yakitoka katika bwawa hilo na kuingia Mto Aprepre ambao, ule ambao nao unatiririsha maji yake kwenda kwenye mito minne ya Egya Nsiah, Bemanyah, Manse na Ankobra.

Hiyo ilimaanisha kwamba maji hayo yalikuwa yakiathiri afya za wananchi wanaoishi huko Dumasi na miji mitatu ya Goloto, Juaben na Egyabroni na pia, wakazi wa mji huo pamoja na vijiji vinavyouzunguka walikuwa wakilishwa kaa pamoja na samaki wanaokufa wenyewe, kutokana na sumu iliyopo kwenye maji ya Mto Aprepre mbali na viumbe hai wengine waliokuwa wanaokotwa wakielea juu ya maji.

Kampuni ya Golden Star Resources Bogoso/Prestea Limited ilipewa jina hilo kutokana na kuwa kwake mjini Prestea, mji ambao upo katika wilaya ya Prestea Huni-Valley iliyopo Magharibi mwa Ghana.

Upo umbali wa Kilomita 50 Kaskazini mwa Pwani ya Bahari ya Atlantiki na katika ukingo wa Mto Ankobra, kiasi cha Kilomita 100 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Cape Coast. Unapitiwa pia na reli inayouunganisha mji huo na ule wa Tarkwa, kisha inakwenda na kuishia katika jiji la Sekondi-Tokoradi.

Pamoja na kuwa na kampuni hiyo iliyochangia uharibifu wa mazingira, Prestea Huni-Valley ipo eneo la ukanda wa misitu inayopata mvua nyingi huku hali yake ya hewa ikiwa ya kitropiki.

Mazingira hayo yanaifanya ipate mvua mara mbili kwa kuanza na vuli zinazonyesha kuanzia Septemba hadi Novemba, kisha zinafuatiwa na za masika zinazoanza mwezi Machi na kuendelea mpaka Julai na kutokana na hali hiyo, wastani wa mvua inazopata ni za milimita 187.83 kwa mwaka.

Mbali na majira ya mvua pamoja na kiwango chake, wilaya hiyo pia ina mazingira yenye joto kali kila siku. Wastani wa jotoridi linalopatikana huko ni kati ya nyuzijoto 26 mpaka 30 za sentigredi.

Kana kwamba haitoshi, utafiti mwingine uliofanywa katika mji wa Dumasi ulibaini kwamba kiwango kikubwa cha zebaki kilichopo chini ya ardhi kiliaathiri pia maji, samaki kwenye mito pamoja na viumbe hai wengine.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Prestea wakati wa utafiti huo walieleza kwamba walikuwa wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya kutibu maji ya kunywa, kupikia, kuoga na kufulia nguo zao yanayochimbwa kutoka chini ya ardhi kwa maana ya visimani.

Ili kupata maji salama yasiyokuwa na kemikali za madini hayo ya zebaki, wananchi hao walikuwa wakilazimika kuchimba visima vyenye urefu wa kuanzia mita 80 na kutumia gharama kubwa zaidi za raslimali fedha.

Mradi huo ulikuwa ukigharamu kiasi kisichopungua cedi 12,000 za Ghana ambazo ni sawa na Dola 3,500 za Marekani, fedha ambazo pia ni wastani wa Shilingi 7,840,000 za Kitanzania ili kukamilisha uchimbaji wa kisima angalau kimoja, kuweka pampu ya kuvuta maji kutoka chini ardhini na kununua na kuweka bomba na tanki la kuhifadhia maji hayo.

Hali hiyo ilitokana na uchafuzi wa mazingira uliosababisha maji katika idadi kubwa ya mito kutokuwa tena salama kwa matumizi hasa ya majumbani, kunywesha mifugo au katika shughuli nyingine za kijamii.

Maeneo mengine yaliyokuwa hatari ni ukanda maarufu wa madini ya dhahabu wa Ashanti na Obuasi, kule ambako vyanzo mbalimbali kama vile mikondo ya maji, visima vya asili pamoja na mabonde navyo viliathirika pia.

Sehemu ambazo mazingira yake yameathirika zaidi ni pamoja na maeneo ya Bondaye, Nankaba, Ashtown, Ankobra na Anfegya yaliyokuwa na uoto wa asili wa kijani unaovutia, lakini ambao hivi leo haupo tena kutokana na uchimbaji huo wa madini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here