Binadamu anaona uzito wa thamani ya uhai?

0

Na Igamanywa Laiton

INASEMEKANA, kwa kila Atomu moja ya uraniamu, ni sawa na risasi moja yenye uwezo wa kupenya kila aina ya kizuizi iwe ukuta, mawe au chochote kile.

Risasi zenye sifa ya miale ya X-Ray, risasi ambazo zikikupata hupenya katika mwili mithili ya sindano ndogo na kuujaza sumu ambayo huanza kuunyonyoa na kuudhofisha mwili.

Hatua hiyo inaelezwa, inachukua muda mchache na ndani ya siku mbili au tatu baada ya mateso makubwa, mauti hufuata.

Fikiria matilioni hayo ya risasi yakivuja na kutapakaa hewani, Kilomita chache kuelekea katika mji wenye wakazi zaidi ya 50,000.

Kwanza, serikali baada ya kutambua janga hilo, inaficha na kujaribu kulishughulikia jambo hilo kimya kimya kwa sababu za kisiasa.

Kwa kuwa mambo yanayofanywa kimya kimya bila msaada kutoka nje, yanakuwa mabaya zaidi, idadi ya vifo inafichwa na miale hatari inazidi kusambaa zaidi katika anga na hatimaye kuanza kuonekana katika anga la nchi ya jirani.

Hatimaye, baada ya takribani siku tatu, serikali inainua mikono juu na kulia kilio cha kuomba msaada. Hivyo, ndivyo mambo yalivyokuwa huko Ukrania, enzi hizo ikiwa chini ya Umoja wa Kisovieti (USSR) kuanzia Aprili 25 hadi 28, mwaka 1986.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wataalamu walipokuwa wakifanya majaribio kama ada ili kuhakiki usalama na ufanyaji kazi wa mitambo katika kinu cha nyuklia cha uzalishaji umeme, kilichokuwa kikipatikana katika mji mdogo wa Pryipat.

Ni mji unaopatikana katika nchi ya Ukrania huko Ulaya Mashariki, Kilomita 16 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Chinobo. Haijulikani kama walifanya makusudi au la! Kwani wataalamu hao waliamua kutofuata kanuni maalumu za kiusalama.

Bila kupiga picha hatari inayoweza kutokea, kwanza wataalamu hao walizima kwa makusudi mfumo wa dharura wa kiusalama wa mitambo waliyokuwa wakiifanyia majaribio.

Pili, bila wasiwasi ila kwa mazoea waliendelea kushughulikia mitambo hiyo yenye uhitaji wa uangalifu wa hali ya juu, huku ikiwa bado ikizunguka na kufanya kazi.

Yaani, ni kama vile kufungua boneti la gari huku ikitembea. Katika uzembe huo mambo yakaenda mrama ilipofika Saa 7 na dakika 23 baada ya kutokea kwa hitilafu katika kiini cha mtambo.

Milipuko kadhaa ikafuata na kusababisha kuvuja kwa miale hatari na hatimaye kutorokea hewani. Katika mlipuko huo, watu wawili walipoteza maisha papo hapo.

Juhudi kadhaa zilifanywa na Mamlaka kwa kuagiza zimamoto kushughulikia moto na kuagiza helikopta imwage kemikali juu ya kinu, ili kuzuia moto na kusambaa kwa miale hatari iliyokuwa ikiendelea kuvuja na kutoroka katika kiini cha uraniamu kilicholipuka.

Kulingana na baadhi ya vyanzo, inasemekana vifo viliendelea kuongezeka, ila serikali ya Sovieti haikutaka dunia ijue kilichokuwa kikiendelea, hivyo ikafanya siri.

Wakati miale ikiendelea kusambaa katika anga, mji wa Pryipat wakazi wake zaidi ya 50,000 walikuwa katika hatari, kwani serikali ya Sovieti ilikuwa bado haijatoa agizo la kuondolewa kwa watu na kupelekwa mahala salama.

Yote hiyo ni kujaribu kuficha juu ya kilichokuwa kikiendelea huko katika kinu cha Chinobo (wakazi hao walihamishwa kisiri Aprili 27 masaa 36 toka kinu kilipuke).

Aprili 28, miale hiyo hatari iliyokuwa ikivuja Chinobo, ilifika Sweden baada ya kupeperushwa na upepo. Kufika kwa miale hiyo nchini humo, kulizusha maswali juu ya kile kilichokuwa kikiendelea huko Sovieti.

Hatimaye siku hiyo hiyo, serikali ya Sovieti ikakiri kuwa kuna msiba katika Chinobo na kuomba msaada wa kushughulika na ‘muuaji’ yaani ile miale hatari iliyokuwa ikiendelea kuvuja katika kinu, asilimia 30 ya tani ujazo 190 za uraniamu zilizokuwa katika kinu cha Chinobo zilikuwa tayari katika anga.

Kufikia Mei 4 mivujo yote ya gesi ilikuwa tayari imeshughulikiwa na mnururisho kukoma. Inasemekana takribani watu 50 walikufa moja moja kutokana na msiba mzima, japo serikali yenyewe ilitoa idadi kuwa ni 28.

Msiba ulikuwa haujaisha kwa idadi hiyo, kwani madhara na vifo ilikuwa ni ya kudumu na tayari mnururisho wa miale hatari ulikuwa umeshatapakaa katika anga, ardhi na katika viumbe hai.

Madhara yalikuwa ni ya kudumu, kwani mamia ya watu ambao moja kwa moja au isivyo walikuwa tayari wamepata kansa, wengi wakiwa wameathirika na kansa ya koo.

Madhara hayakuishia kwenye vifo na kansa, kwani msiba mzima uliicha serikali ya Sovieti taabani kiuchumi, kwani mpaka mwisho zoezi zima la kushughulikia janga hilo ulikuwa umeigharimu takribani Dola za Kimarekani Bilioni 235.

Ukiachana na hilo, nchi ya Belarusi pekee ilikuwa imepoteza nusu ya ardhi yenye kufaa kwa kilimo, wakati huo huo ikitumia takribani asilimia 22 ya jumla ya bajeti yake kushughulika na madhara ya msiba huo. Msiba huo uliharakisha kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti kwa namna fulani na hatimaye kuisha kwa vita baridi.

Kilichotukia Chinobo, kinazusha maswali ya msingi ambayo ni ‘Je binadamu tayari amepevuka katika kutumia teknolojia? Je, teknolojia hizi zinazotuzunguka madhara yake yanaeleweka hakika?

Huku swali lingine la msingi likiwa ni; Je, binadamu anaona uzito wa thamani ya uhai? Kama ndiyo, basi ni kwanini huona maslahi ya kisiasa kuwa na thamani kuliko uhai?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here