Idara ya habari Maelezo Z’bar yawaaga wastaafu

0
Mwenyekiti wa Bodi ya Idara Habari Maelezo Yussuf Omar Chunda akimkabidhi Zawadi ya Fedha Taslim aliekua Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Hassan Khatibu Hassan katika hafla ya kuwaaga Wastaafu wa Idara hio hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Zanzibar.

Na Sabiha Khamis, MAELEZO

MWENYEKITI wa Bodi ya Idara Habari Maelezo Zanzibar Yussuf Omar Chunda amewataka wafanyakazi kuwa na nidhamu wanapokuwa kazini ili kuwajengea heshima wanapofikia kustaafu.

Wito huo ameutoa katika hafla fupi ya kuwaaga wafanyakazi wawili wa Idara hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo alisema, nidhamu inapodumu kwa mfanyakazi hupelekea mashirikiano mazuri kwa wafanyakazi wengine.

Aidha, amewataka wastaafu hao kuendelea kutoa mashirikiano kwa pale ambapo wanahitajika kwa ushauri na mapendekezo iwapo wakiwa nje ya ofisi

Ameeleza kuwa, wafanyakazi waliobakia kazini wanapaswa kufuata nyayo za wastaafu hao kwa kufanyakazi kwa weledi ili kupatikana ufanisi.

Nae, Katibu Mkuu wa Vyama vya Wafanyakazi Khamis Mwinyi Mohamed amewaomba wafanyakazi kujiunga na umoja wa vyama vya wafanyakazi jambo ambalo litawasaidia kutatua changamoto zao.

Ameeleza kuwa, Umoja ndio daraja la kupatikana kwa fursa ambazo zitawawezesha Wafanyakazi kushiriki katika kutoa changamoto zao kujadili mambo yao mbali mbali wanayokumbana nayo katika sehemu zao za kazi ili kupatiwa msaada.

“Wafanyakazi wakipata changamoto kazini Chama cha Wafanyakazi ndio watetezi wao tunahakikisha inapatikana suluhisho la tatizo hilo” alisema Katibu Khamis.

Hata hivyo, ameishukuru Idara hiyo kwa kuwaunga mkono vyama vya wafanyakazi katika kutatua changamoto za wafanyakazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mstaafu wa Idara Habari Maelezo Zanzibar Hassan Khatib Hassan amewashukuru Viongozi wa Idara hiyo kuendeleza utamaduni wa kuwaaga wafanyakazi wake wanapostaafu jambo ambalo huwapa moyo na faraja.

Aidha, amesisitiza nidhamu, uadilifu na heshima katika kazi na kuwataka wafanyakazi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili wanapostaafu waweze kujiendeleza.

Chama cha Wafanyakazi kimemkabidhi cheti cha heshima cha uchangiaji bora Mfanyakazi Sikudhani Said ambae amechangia kwa miaka 40.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here