Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuhakikisha vifaa vya TEHAMA zinapatikana kwa wingi na vikiwa na ubora, Tume ya TEHAMA (ICTC) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) la kuanzisha maabara itakayohusika katika kutengeneza, kuunganisha na kukarabati vifaa vya Tehama kwa ajili ya soko la Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Imesisitizwa, lengo ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazotegemewa katika uuzaji wa bidhaa za TEHAMA barani Afrika.
Makubaliano hayo yalitiwa saini jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo.
Akizungumzia makubaliano hayo, Dkt. Mwasaga alisema ni hatua muhimu katika kuipa heshima Tanzania katika eneo la teknolojia kutokana na mafanikio makubwa iliyopata eneo la utengenezaji wa mifumo ya mawasiliano.
Alisema, kutia saini kwa makubaliano ni hatua kubwa inayofikiwa na Tanzania, kwa kuwa imepata mafanikio katika utengenezaji wa mifumo kutokana na ubunifu uliofanyika na sasa malengo ni kufikia hatua ya nchi inayouza bidha za TEHAMA ndani na nje ya nchi.
“Tunachokifanya leo ni kikubwa sana, Tanzania tumefanya ubunifu mkubwa wa kutengeneza mifumo na sasa tunaelekea kufikia nchi inayouza bidhaa za TEHAMA ndani ya nchi na nje. Sisi tunaamini tukifanya bunifu zetu vizuri tutafika,” alisema.
Alieleza; “Ushirikiano na TIRDO ni hatua kubwa kwa kuwa ni moja ya taasisi ya serikali yenye nguvu zaidi, kushirikiana nao inatuongezea nguvu zaidi hasa kutokana na jukumu la Tume ni kufanya tafiti ambapo hubadilisha kuwa teknolojia na baadaye inakuwa ufumbuzi.”
Alisema, ana matumaini makubwa ushirikiano huo, utasaidia kutoa tija kubwa katika eneo la ubunifu wa Tehama na kusaida kufikia malengo ya kuhakikisha nchi inafikia uchumi wa kidijitali kutokana na kuweza kufanya utafiti, ujasiriamali na ubunifu.
Kwa upande wake, Profesa Mtambo alisema, makubaliano waliyosaini yanawakilisha maono ya pamoja na kujitolea kuanzisha kwa vituo vya kukuza bunifu za TEHAMA vya kisasa ndani ya eneo hilo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo, nimefarijika kwa kuingia makubaliano ya kushirikiana katika kuanzisha maabara ya kutengeneza na kukarabati vifaa vya teknolojia Tanzania” alisema.
Aliongeza; “Naipongeza Tume kuona sisi ni watu muhimu kushirikana, nimekoshwa sana na kuja hapa hapa ni jambo bora sana kwetu maabara itakapoanzishwa ni mahala sahihi”.
Alieleza “Nawapongeza kwa wote wenye mawazo haya hadi kuja na wazo hili. Naomba ushirikiano huu kwa TIRDO na Tume ya TEHAMA uendelee na juhudi hii iliyoanza idumu zaidi”
Hivyo, alisema ana matumaini makubwa uwepo wa mabara hiyo utasaidia kukuza ajira kwa vijana kupitia ubunifu na taifa kunufaika.
Makubalino hayo yamekuwa siku moja baada ya Tume ya TEHAMA kuingia makubaliano na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) ili kuanzisha vituo vya ubunifu katika mikoa mbalimbali nchini, lengo ikiwa kuharakisha kufikisha ujuzi wa TEHAMA kwa wananchi.