Na Mohamed Kazingumbe
WAYAO asili yao ni majimbo ya Kusini mwa Tanzania katika wilaya ya Newala (kidogo), Masasi, Nanyumbu na Tunduru. Hapana shaka tukisema majimbo ya Kusini mwa Tanzania, yanapakana na majimbo ya Kaskazini ya nchi jirani za Msumbiji na Malawi.
Desturi na mila za Wayao hao ambao wanatenganishwa na ukanda mwembamba wa Mto Ruvuma katika mipaka ya kimataifa ya nchi za Msumbiji, Malawi na Tanzania. Bila kujali huyu ni Mtanzania, Msumbiji au Mmalawi wote wanaasili moja.
Utamaduni mmoja, ngoma, mavazi, lugha; wanatembeleana kijadi bila bughdha ya kimipaka. Nadhani hii ndio sababu hata serikali zenyewe zinafahamu, lakini ili mradi hawavunji sheria mama za kila nchi.
Hata hivyo, makala yetu ni juu ya somo la ‘ngoma’ ya Wayao ya ‘masewe’. Maelezo yaliyonogeshwa ni kuonyesha jinsi kabila hilo lilivyosambaa maeneo mengi Kusini mwa Tanzania hadi nchi jirani za Msumbiji na Malawi.
Jamaa hawa ni hodari katika kulinda na kuendeleza utamaduni wao wa asili. Ni kweli kama mgeni akifika majira za mavuno au nyakati za sherehe za unyago na jando au kumsimika chifu (Mwenye), atashangaa kuona heka heka zinavyotikisa jamii.
Wanawake kwa wanaume hawatoshi katika kunengua kwenye ngoma hiyo ya masewe. Hapa ni ‘mshikemshike tu nguo kuchanika’ jinsi kundi la wacheza ngoma hiyo wakiwa wamevalia vibwaya kiunoni, njuga au kokwa za embe miguuni na kofia zilizopambwa kwa manyoya ya ndege wakubwa.
Mara nyingi mbali ya wanaume waliovaa kofia zenye kupambwa kwa manyoya marefu ya ndege, pia wengine wao wanavalia kofia za ukindu (miaa). Sura za wachezaji hao wake kwa wanaume hupambwa kwa poda rangi nyeupe na nyekundu.
Hali kadhalika safu ya wanawake nayo ni ya mfano wakipekee, kwani wao hujiweka nadhifu kwa kuvaa sare ya kaniki, kujifunga kitambaa cheupe kifuani na kiunoni huku wakiwa wamebeba majembe au nyungo. Hii ni ishara ya sherehe hiyo kuwa ya mavuno na kilimo.
Milindimo ya ngoma ya Masewe hutokana na zama maarufu kama “Msondo” ikiungwa mkono ala zingine na chuma kinachogongwa na kuleta mchanganyiko wa mvumo wenye kusisimua wachezaji kufanya vitu vyao. Zana hizo huleta raha na burudani sio tu kwa watazamaji wanaofurika katika hafla hizo, bali huwa ni furaha ya pekee.
Ngoma hiii ya Masewe ni moja ya ngoma mashuhuri Tanzania kutoka Kusini mwa nchi, hususani katika Wilaya za Masasi na Tunduru.
‘’Sherehe zote ya kitaifa Masewe ndio chaguo,’’ mkazi wa Chanika – Nyeburu , jijini Dar es Salaam, Mohamed Chilamboni, alimwambia mwandishi wetu, alipotaka kufahamu ukweli wa ngoma hiyo.
Chilamboni, anakumbuka zama za machifu (Mwenye) huko kwao Tunduru ambapo ngoma ya Masewe ilikuwa burudani ya kuburudisha jamii kabla na baada mkuu kuhutubia, aliongezea.
Mvuto mkubwa kwenye ngoma hii ni madoido ya mashairi yanayotolewa hususani wanaoongoza kuimba. Kiongozi wao hujitokeza mbele, huku wengine wakiwa wametulia na pia mapigo ya zana yakiwa yamepunguzwa ili kutoa nafasi kwa kiongozi huyo atoe mashairi ambayo huleta burudani kwa watazamaji.
Manjonjo ya wachezaji wanaume na wanawake ni hali tosha kuwa utamaduni wa Wayao ni silaha kubwa katika kukimbiza tamaduni za kigeni nchini Tanzania. Wakati mwingine unaweza kujiuliza, ni kwa nini Waafrika wanashindwa kutazama walikotoka na kutelekeza ngoma zao tamu?
Mara baada ya uhuru mwaka 1961 Disemba 9, kulikuwa na vikundi vingi vya Watanzania ambavyo vilikuwa vimejikita kudumisha sanaa ya maonyesho ya ngoma asili ikiwemo kikundi cha taifa. Vilikuwa mahodari katika kukusanya na kuhifadhi aina ya ngoma ambazo wageni wote wa Serikali waliburudishwa mara baada tu ya kutua kwenye uwanja wa ndege.
0715 687454