Na Abel Kiharo
UMEWAHI kusikia mwanadamu alivyo na uwezo mkubwa wa kuamua aina ya matokeo anayoweza kuyapata katika maisha yake mwenyewe? Kama jibu ni ‘ndiyo’ basi hongera sana na kama jibu ni ‘hapana’ basi karibu upate kitu kipya katika makala hii.
Kila mwanadamu ameumbwa na uwezo wa kufikiri, kuongea, kisha uwezo wa kutenda. Ni wanadamu wachache mno ambao hawana uwezo wa kuongea! Kwa kawaida, tunategemea kila mwanadamu awe na uwezo wa kuwaza, kuongea na kutenda.
Aina ya maisha uliyonayo sasa ni matokeo ya aina ya mawazo ambayo umekuwa ukijiwazia, mawazo hayo ndiyo ambayo yameamua aina ya maneno yanayokitawala kinywa chako na maneno hayo ndiyo yaliyozalisha matendo yako na hatimae matendo yako ndiyo yamekuwa mwamuzi mkuu wa aina ya matokeo uliyonayo maishani mwako.
Mawazo yako ni mfano wa mbegu katika maisha yako, maneno yako ni mbolea na matendo yako ni maji ya kuiotesha mbegu ile uliyoipanda maishani mwako (yaani mawazo unayojiwazia!).
Chochote unachokitaka katika dunia hii utakipata ikiwa utakubali mawazo yako yatawaliwe na kitu hicho, maneno ya kinywa chako yakiri ushindi juu ya kitu hicho na matendo yako yawe mchochezi mkuu wa kukufikisha kwenye kitu hicho.
Unaweza ukawa bora ikiwa mawazo yako yatakuwa bora, kwa kuwa maisha ya mwanadamu ni matokeo ya mawazo yake mwenyewe.
Mwanadamu ambaye ana maisha bora, hujiwazia mawazo yaliyo bora siku zote, hujitamkia maneno bora nyakati zote hali ambayo inachangia matendo yake yawe bora.
Hii ndio kanuni kuu ya kuleta matokeo katika maisha yetu, kanuni hii inasema “Hauwezi kupata nje ya vile unavyojiwazia, wala hauwezi ukaamini kinyume na aina ya mawazo yaliyoitawala akili yako.” Hii ndiyo sababu watu wengi huishia kupata matokeo mabaya maishani mwao.
Watu wengi wanadhani hawawezi kufika mbali kimaisha, mawazo hayo yanasababisha hata maneno yao yawe ni ya kujidharau matokeo yake hata matendo yao huishia kuwa ya uvivu na kujikatia tamaa.
Kama unataka kubadilisha aina ya matokeo unayoyapata maishani mwako, anza kwanza na kubadilisha aina ya mawazo unayojiwazia, baada ya hapo uhakikishe maneno yako yanaendana na mawazo hayo.
Ukikamilisha kwa kuyafanya matendo yako kuendana na maneno yako, hapo utakipata kile unachokitaka. Hauwezi ukafanikiwa kuyabadilisha matendo yako ikiwa maneno yako hayajabadilika, wala hautayaona matunda yoyote bora maishani mwako ikiwa hautakubali kuyabadilisha mawazo yako.
Mbegu ndiyo huamua aina ya matunda yatakayopatikana; vivyo hivyo mawazo yako ndiyo yatakayoamua aina ya matokeo utakayoyapata maishani mwako.
Using’ang’anie kubadilisha matendo yako ikiwa bado haujabadilisha namna unavyowaza. Mawazo yako ndiyo huamua mtazamo wako juu ya mambo, na mtazamo wako ndiyo huamua imani yako juu ya mambo hayo.
Kama unatamani upate matokeo makubwa, anza kwa kuwaza mawazo makubwa, uendelee kwa kuongea maneno makubwa na ukamilishe kwa kufanya mambo yako kwa namna ya ukubwa.
Mwanadamu ndiye kiumbe pekee aliyependelewa zaidi hapa duniani, hii ni kwa kuwa mwanadamu ameubeba uwezo mkubwa ndani yake wa kuchagua. Kwahiyo, upo huru kuchagua ama uishi maisha bora au maisha mabovu.
Chochote utakachokichagua ndicho utakachokipata, ukichagua kilicho bora utapata kilicho bora na ukichagua kibovu utaishia kukipata kilicho kibovu.
Siku zote wakumbuke hawa mapacha watatu ambao ni wazo, neno na tendo. Kama utawafanya mapacha hawa waongee lugha moja na lugha hiyo ikawa ni bora, kwa hakika hautaweza kukwepa kuyapata matokeo bora katika maisha yako.
Lakini, kama ukishindwa katika hilo, maisha yako yataendelea kuzalisha matokeo ambayo hata wewe mwenyewe hauyapendi. Ukiwaza kile unachokipenda, ukakiongea zaidi kile unachokipenda na ukakamilisha kwa kukifanya kitu hicho unachokipenda, mwisho utaishia kupata matokeo unayoyapenda.
Yule mtu aliyelijenga lile ghorofa refu, jengo lile lilianzia kichwani kama wazo, baada ya hapo wazo hilo likaanza kuutawala mdomo wake na mwisho wa siku akalikamilisha wazo hilo kwa kulifanyia kazi! Mchawi mkubwa wa maisha yako ni yale mawazo mabaya unayojiwazia juu ya maisha yako mwenyewe.
Kikwazo kikubwa kinachokuzuia kupata chochote unachokitaka maishani mwako, ni mawazo yako mwenyewe. Sababu kubwa kwanini haufiki mbali kwa kupitia mambo yale uyafanyayo ni mawazo yaliyoitawala akili yako, ambayo yanakufanya uamini haustahili hata kidogo kufika mbali.
Akili ya mwanadamu ni sawa na silaha ambayo, kama isipotumiwa vyema badala ya kumuangamiza adui itaishia kumuangamiza muongozaji wa silaha hiyo!
*Mwandishi wa Makala hii ni Mkufunzi wa Vijana na Mjasiriamali. Kwa maoni, ushauri au maswali usisite kuwasiliana naye kwa anuani zifuatazo:- Barua pepe: kiharoabel@yahoo.com. Simu na WhatsApp: +255767180002 /+255628733839. Mitandao ya Kijamii: https://linktr.ee/abelkiharo.