‘Hatutaruhusu watanzania waumizwe na Wanyama’

0
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana.

Na Iddy Mkwama

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema, moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wanalinda maisha ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.

Alisema hayo hivi karibuni wakati akipokea magari na mitambo ambayo imetolewa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kupitia Mradi wa kupunguza athari za UVIKO 19 “Emergency and Recovery Support for Biodiversity Tanzania (ERB)” ambao upo chini ya Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).

Waziri Chana alisema, watahakikisha wanadhibiti mwingiliano wa Wanyama na binadamu ili wananchi wawe salama kwa kununua vifaa vya kisasa zikiwemo ndege nyuki (drones) na vingine ambavyo vitawekwa kwenye maeneo hayo.

“Tutaendelea kuhakikisha tunadhibiti mwingiliano wa binadamu na wanyama hususani tembo, hili suala ni miongoni mwa vipaumbele vyetu ili wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi wawe salama na hifadhi zetu ziwe salama,” alisema Dkt. Chana.

Aliendelea kusema: “Hatutaruhusu watanzania waumizwe au waletewe madhara na Wanyama, ambapo tunaweza kuona namna gani ya kuwadhibiti, pia nitoe rai kwa wakuu wa mikoa na wilaya, yale maeneo ambayo wanyama hususani tembo wanapita, pamoja na jitihada za kuokoa shoroba, yatambuliwe ili yasitumike kwa ajili ya mashamba na makazi.”

Alisema, moja ya mambo yanayoweza kufanyika ni kuweka shughuli ambazo zitasaidia hifadhi, “nipongeze maeneo yote ambayo jamii wametenga maeneo ya uwekezaji, vijana wanapata ajira, vijiji vinapata mapato na inasaidia kudhibiti Wanyama wasiende kuwadhuru wananchi.”

Waziri Dkt. Chana alisema, viongozi wa maeneo ambayo yapo pembezoni mwa hifadhi wachague shughuli ambazo ni rafiki kwa hifadhi, “tusiweke mashamba ambayo Wanyama watapita kukanyaga au kula,”

“Tusiweke makazi kwasababu Wanyama watafika maeneo yale na kuleta madhara. Ni muhimu kuwa na maeneo nje ya hifadhi kwa ajili ya kulinda wanyama na wananchi wapate faidia.”

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority – TAWA) katika kipindi cha miaka mitatu, inaonyesha kuwa Mamlaka hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaepusha wananchi na madhara yanayotokana na Wanyama huku ushirikishwaji wa wananchi ukiongezeka.

Taarifa inaonyesha kuwa, kutokana na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kati ya mwaka 2021-2024 TAWA imefanya jumla ya doria siku watu 58,818 kukabiliana na matukio 8,001 yaliyotokea katika Wilaya 73 nchini.

Jitihada nyingine zilizofanyika ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kujenga vituo vituo 16 vya askari katika Wilaya 16 ili kuitikia kwa haraka matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, ununuzi wa pikipiki 50, kutoa mafunzo na kushirikisha askari wa wanyamapori wa vijiji; Village Game Scout na jeshi la akiba wapatao 184.

“Askari waliopata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanafanya kazi kwenye maeneo sugu ya matukio (Bunda, Busega, Meatu, Same, Lindi, Korogwe, Itilima, Liwale, Nachingwea, Mwanga, na Tunduru); Kuongeza vituo vya muda vya askari (ranger stations) kutoka 46 hadi 55; Kuongeza idadi ya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kutoka 139 hadi 237” alisema Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori “TAWA) Mabula Misungwi wakati alipotoa taarifa ya utendaji ya Mamlaka hiyo kwa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliendelea kusema: “Tumeimarisha vikundi 179 vya wananchi vya kufukuza tembo na kutoa vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo Roman candles 1,320, thunder flashes 1,310, vuvuzela 548, filimbi 288, tochi 524, mbegu za pilipili, mabomu ya pilipili”

“Tumefunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo 8 katika Wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwe na kuimarisha mawasiliano kwa kutoa namba ya kupiga simu bure ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa mapema.”

Kutokana na jitihada hizo, Kamishna Misungwi alisema, madhara hasi ikiwemo idadi ya vifo imepungua kutoka vifo 318 kati ya mwaka 2017-2020 hasi vifo 259 kati ya mwaka 2021- 2024 licha ya kuongezeka kwa matukio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here