MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni amesema, kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025, kiasi cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia futi za ujazo Bilioni 301.33.
Alisema, kati ya kiasi hicho, futi za ujazo Bilioni 142.35 zilizalishwa kutoka Kitalu cha Mnazi Bay na futi za ujazo Bilioni 158.98 kutoka Kitalu cha Songo Songo. Uzalishaji huu ni wastani wa futi za ujazo Bilioni 35.59 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo Bilioni 39.74 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.
Mhandishi Sangweni alisema hayo kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa habari uliofanyika leo, Mei 19, 2025, ambapo alisema kwa kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi ulikuwa wastani wa futi za ujazo Bilioni 32.03 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo Bilioni 25.13 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.

“Gesi asilia iliyozalishwa ilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme; matumizi ya viwandani, majumbani, taasisi, na
katika magari. Kwa mujibu wa mikataba ya PSA, mwekezaji hutumia fedha zake katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambapo akikosa huwa anarudisha eneo kwa Serikali na kuondoka.
“Lakini, pindi akipata mafuta au gesi asilia fedha zipatikanazo baada ya mauzo ya rasilimali iliyopatikana hulipa mrabaha, hurudisha mtaji aliowekeza, hulipa kodi na tozo mbalimbali na kinachobaki hugawiwa kwa wabia wa mkataba ikiwemo Serikali na TPDC” alisema Mhandisi Sangweni.

Alisema, kutokana na utaratibu huo, ni muhimu PURA kuhakiki kiasi cha fedha kinachowekezwa pamoja na shughuli zinazotekelezwa ili kuepuka udanganyifu unaoweza kufanywa na mwekezaji ambapo wameendelea kuhakiki na kukagua mapato na gharama za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji katika mikataba ya ugawanaji mapato kati ya Serikali na waendeshaji wa Vitalu (PSA auditing) ili kuhakikisha Serikali inapata mgawo stahiki kwenye mapato ya mafuta na gesi asilia.
“Kupitia kaguzi hizi zaidi ya Shilingi Bilioni 340 zimerejeshwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na wawekezaji katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita. Fedha hizi zingeweza kutumika kama marejesho ya mtaji wa mwekezaji,” alisema.
Aidha, kupitia mkutano huo ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Mhandisi Sangweni alisema, katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali kupitia PURA imeendelea na maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

“Kama nilivyoeleza, zoezi la kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2013. Kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili na kwa ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia kutekeleza zoezi hili muhimu,” alisema Mhandishi Sangweni.
Akitaja baadhi ya faida za kunadi vitalu hivyo, Mkurugenzi huyo wa PURA alisema, itasaidia kuongezeka kwa ugunduzi na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kukuza uchumi wa nchi kutokana na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia.
Pia, kuwezesha upatikanaji wa data za petroli utakaoongeza wigo wa taarifa zitakazosaidia katika kuchochea utafutaji zaidi wa mafuta na gesi asilia nchini, na kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania na matumizi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wafanya biashara na watoa huduma wakitanzania.