Dkt. Mwinyi: SMZ inatambua mchango wa kambi za matibabu na uchunguzi

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na kambi za matibabu na uchunguzi wa afya, kwani zinaisaidia Serikali kupunguza gharama za wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa nje ya nchi kutibiwa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Julai 21, 2025, alipoifungua Kambi ya Matibabu ya Kumbukumbu ya Hayati Ali Hassan Mwinyi, Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru madaktari bingwa kutoka Kenya na Marekani kwa uamuzi wao wa kuja Zanzibar na kushirikiana na madaktari wazalendo kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni sadaka ya kumuenzi Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanya juhudi kubwa za kuleta mageuzi makubwa katika kuimarisha sekta ya afya ili wananchi wapate huduma bora za matibabu.

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuimarisha majengo na miundombinu ya sekta ya afya, kuongeza wataalamu wabobezi, pamoja na kuimarisha maslahi yao.

Ameishukuru timu ya madaktari bingwa kwa kumuenzi Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa vitendo kupitia matibabu hayo. Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alizuru kaburi la Hayati Ali Hassan Mwinyi pamoja na kumuombea dua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here