DCEA, TAKUKURU kushirikiana mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya

0

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), zimekubaliana kushirikiana kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita vitendo vya rushwa nchini.

Taasisi hizo zimefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa hutumia rushwa kufanikisha usafirishaji wa dawa za kulevya ambapo wamekuwa wakiwahonga watu wasiowaaminifu ili wawasaidie kukamilisha uharifu huo katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Ushirikiano huo utajikita zaidi katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita rushwa kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuoni kupitia club za kupiga vita rushwa mbazo sasa zitatumika kupiga vita rushwa na dawa za kulevya.

Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dodoma, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAKUKURU na kuhudhuriwa pia na baadhi ya Maafisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo alisema, Mamlaka katika kuendeleza mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya Nchini, imeona ni vema ikashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kupanua wigo wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya. 

Alisema, ushirikiano huo ni muhimu kwani utaisaidia sehemu kubwa ya jamii hasa wanafunzi ambao baadhi yao kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya wakiwa katika umri mdogo, kufahamu madhara ya dawa za kulevya na hatimaye kutoshiriki kwenye matumizi na biasha ya dawa hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa CP. Salum Rashid Hamduni, alisema anatambua ushirikiano baina ya taasisi hizo utaleta tija katika mapambano dhidi ya Rushwa na tatozo la dawa za kulevya Nchini.

Pia, alisisitiza kwamba, ni muhimu taasisi hizo zikajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa kwa ufanisi mkubwa huku akifafanua ushirikiano huo usijikite tu katika utoaji wa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya, bali pia katika kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana makosa ya rushwa. “Kwani ni wazi kuwa, idadi kubwa ya watu wanaokutwa na makosa hayo pia hukutwa na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here