Na Lela Muhaji
SERIKALI imesaini makubaliano na Benki ya Dunia ya Mkopo nafuu wa Shilingi Trilioni 1.24 kwa ajili ya ujenzi wa uendelezaji wa bonde la Mto Msimbazi utakaohusisha ujenzi wa daraja la kisasa la Jangwani pamoja na miradi ya umeme vijijini.
Ujenzi wa daraja la kisasa la Jangwani, unatajwa kuandika historia nyingine ya daraja bora na la aina yake kama la TANZANITE lililopo baharini, ambapo nalo litajengwa maeneo ya jangwani na hivyo wakazi wa Dar es Salaam kusahau adha ya mafuriko.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mara baada ya hafla ya makubaliano hayo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, alisema mikataba hiyo miwili yenye gharama ya Dola Milioni 535 sawa na Shilingi Trilioni 1.24 itaandika historia na kukuza uchumi wa nchi.
“Huu ni mwanzo kati ya yale makubwa ambayo Rais Samia anatarajia kufanya katika mwaka huu wa fedha ikihusisha ujenzi wa miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam,” alisema.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo ni mwendelezo wa kuaminika Kimataifa kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo kwa sasa nchi inaaminika zaidi hali inayosababisha majadiliano ya fedha na uendelezwaji wa miradi ya kiuchumi kukubalika kila sehemu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, alisema ujenzi wa daraja la juu la kisasa litakalofanana na la Tanzanite lililopo baharini au la Nyerere Kigamboni utaandika historia mpya ya kusahau adha ya mafuriko maeneo ya Jangwani.
Alisema, ujenzi huo utakuwa wa daraja la Mita 390 na litainuka kwa Mita sita na kuhusisha upanuzi wa mto kwa Kilomita 1.8 juu na Kilomita 1.8 chini na kujengewa kingo za zege pembeni.
“Ujenzi utagharimu zaidi ya Dola Milioni 63.3 na hivi karibuni tunatarajia kutangaza tenda ambapo baada ya miezi mitatu hatua za awali zitakuwa zimekamilika,” alisema.
Aidha, Mtendaji Mkuu alieleza kuwa, usanifu wa ujenzi umekamilika ambapo michoro inaonyesha kuwapo na daraja la kisasa utakaohusisha kuondolewa kituo cha mabasi ya mwendokasi Jangwani ambacho kitahamishiwa Ubungo Maziwa.
Hivyo, alisema matarajio ni kuanza ujenzi huo Aprili 2023 na kukamilika baada ya miaka miwili hadi mitatu na kuondoa adha kubwa ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.