CUF watoa pongezi kwa Simba na Yanga

0

THE CIVIC UNITED FRONT(CUF- Chama Cha Wananchi)

SALAMU ZA PONGEZI KUFUATIA TANZANIA KUFANIKIWA KUINGIZA TIMU MBILI ROBO FAINALI CAFCL:

Pamoja na kuwa ni Rekodi Mpya na Kubwa kwa Tanzania kwa mara ya kwanza kuingiza timu mbili kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CHAMPIONS LEAGUE -CAFCL), Tanzania pia imekuwa ni nchi pekee iliyofanikiwa kuingiza timu mbili kwenye hatua hiyo mwaka huu kwa Bara zima la AFRIKA. Hii ni hatua kubwa kabisa inayoashiria kukua kwa Soka la Tanzania.

Tunazipongeza timu za Simba na Yanga; ikiwa ni pamoja na Menejimenti, Mabenchi ya Ufundi, Wachezaji na wadau wote muhimu ndani ya Vilabu hivi vikongwe nchini. Tunatoa pongezi hizi ndani ya wiki ya Maombolezo kufuatia Kifo cha Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye wakati wa Uongozi wake aliumizwa na matokeo mabaya ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) na Vilabu vyetu kiasi cha kupelekea atamke kwa uchungu kwamba “Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu” (Kila mtu anaweza kujifunza kunyoa). Muda mfupi kabla ya kifo chake alishuhudia Taifa Stars ikishiriki hatua ya Makundi AFCON, kabla ya hatimaye Simba na Yanga kutinga katika hatua hii ya Robo Fainali CAFCL.

Mafanikio haya yaliyofikiwa katika maendeleo ya Soka nchini ni zao la juhudi kubwa zilizofanywa kwa muda mrefu na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kanali Mstaafu Idd Omar Kipingu aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Makongo na baadae Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT). Mchango wa Mheshimiwa Kipingu kwenye maendeleo ya Soka nchini ni mkubwa sana na unastahili kudhibitiwa kimaandishi ili usiwe HISTORIA inayokufa. Aidha, Mchango wa Wafadhili wakiwemo Marehemu Abbas Gulamali, Azim Dewji, Yusuf Manji, Mohamed Dewji (MO Dewji) na hatimaye Ghalib Said Mohamed (GSM) umeongeza sana kasi ya kukua kwa mchezo huo nchini. Hatuwezi kuhitimisha orodha ya waliofanikisha mafanikio haya bila kuutaja uongozi thabiti wa Shirikisho la Soka nchini TFF (chini ya Wallace Karia).

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuchagiza hamasa kwa wachezaji wa timu zetu kupitia motisha ya kununua kila goli, linalochangia kwenye Ushindi wa timu, kwa shilingi milioni 10. Hili nalo limeongeza ari na hamasa kwa wachezaji na kuchangia kwenye Ushindi wa timu zetu.

CUF- Chama Cha Wananchi tunatamani kuona timu zetu hizi mbili zinakutana Fainali na kuelekea Tanzania inatwaa Ubingwa wa mashindano haya mwaka huu.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Machi 4, 2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here