Na Mwamba wa Kaskazini
NILIKUWA kijijini kwa likizo ndefu kidogo nikawa nasikia sana kuhusu ujio wa dhana mpya ya kisiasa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “4R.”
Dhana iliyojenga, sio mtazamo kwa Serikali tu wala chama chake, bali mwelekeo mpya wa nchi katika kuhakikisha, kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kimataifa, kama kuna mahali kama Taifa tulikosea au kukoseana basi sasa tuitazame kesho yetu kwa jicho la mabadiliko, maridhiano, kustahimiliana na ujenzi wa Taifa jipya.
Siku nilipomuona Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amepewa nafasi kukutana na Rais Samia Ikulu, nilifarijika sana nikaamini kama kuna mtu ameelewa dhana hii alikuwa Mbowe na chama chake.
Kumbe loh salaleee!!! Chadema ni wale wale na miaka nenda rudi; sasa kimekuwa Chama kinachoangalia kinataka nini na sio Taifa linataka nini?
Tangu alipoasisi dhana hii, Rais Samia ameunda Kamati kadhaa za kuchambua masuala ya kijamii ikiwemo Tume ya Haki Jinai na Kikosi Kazi cha kuangalia masuala kadhaa ya kisiasa na mabadiliko ya kisheria.
Kwamba, leo vyama mbalimbali, mabingwa mbalimbali wa sheria za Katiba (constitutional laws) na hata sheria za Kimataifa (international laws) lakini pia Wachumi (economists) na Wanasayansi za siasa (political scientists) lakini pia wakiwemo wanasiasa wenyewe (practising political pundits) wamekaa na kuyaona ya kuanza nayo, hatimaye muswada unakwenda Bungeni, lakini Mbowe anaibuka anataka kuandamana!
Nadhani jamii inaendelea kujionea jinsi wenzetu hawa wasivyosimamia maslahi ya Taifa (manufaa ya walio wengi) na sasa wanaendelea kuonesha taathira ya kuendekeza maslahi yao binafsi!
Ni hawa hawa walitunyima Katiba mpya mwaka 2014/2015 walipojitoa Bungeni si kwa sababu ya Katiba mbaya inayopendekezwa bali kwa sababu masuala yao binafsi hayakupenya tena katika mchakato wa kidemokrasia. Wakaharibu kila kitu.
Nani asiyejua jinsi Katiba ile pendekezwa ilivyokuwa imesheheni masuala ya kimaboresho ya wananchi kama haki za kiuchumi, binadamu na hata za kisiasa ikiwemo uwezekano wa kubanwa Tume ya Uchaguzi katika masuala ya uchaguzi!
Wakati mtaalamu mmoja wa masuala na nadharia ya sheria na jamii (sociological jurisprudence) akiyaita maboresho yale kuwa yalikuwa “hatua kubwa za kuanzia katika kuimarisha demokrasia na utawala wa Sheria Tanzania,” Machadema wao walisusia.
Kwao yote makubwa kwa faida ya wananchi na Taifa kupiga hatua wakati ule hayakuwa na maana wakakimbia Bungeni na kutaka kuanzisha vurugu za kwenda mitaani eti Ukawa sijui Ukuta sijui nini. Bahati nzuri watanzania wakawapuuza.
Leo wanataka kukwaza jaribio jingine la nchi kupiga hatua kisheria na Kidemokrasia. Hawataki kuona maboresho katika mifumo yetu. Wako kule kule, zama zile zile. Tuwakatae.
Namsihi Rais Samia aendelee na kazi kubwa iliyoko mbele yake, awapuuze, madai yao sio madai na mahitaji ya wananchi yamesheheni maslahi binafsi na kutotaka Taifa lisonge mbele.
Wanajifanya hawajui dhana ya mabadiliko katika jamii kuwa ni hatua. Wanajua vyema na wanafahamu hata Katiba ya Marekani na sheria zao hubadilishwa pale matakwa ya Taifa yanavyohitaji sio kelele tu au kila kitu kitafanyika wakati mmoja.
Ndio maana Katiba ya Marekani imeshabadilishwa mara 27 sasa. Maana yake ni nini? Hakuna badiliko moja au muswada mmoja unaoweza kubadilisha kila kitu kwa wakati mmoja, mabadiliko ni taratibu, ni hatua na ni mchakato; leo unaboresha hili kesho lile kwa uzoefu huu au ule.
Chadema kuleta shinikizo la kutoka kwenye mchakato wa Kibunge unaoendelea ambako wadau wanatoa maoni na kutaka kuandamana ni utoto, ni kurudi kule kule, ni kuturudisha nyuma. Tuendelee kuwakataa.
Ndio maana makala yangu haya leo yanahoji tu kwa yote haya hawa jamaa zetu kutaka kuandamana wanasimamia maslahi ya Taifa (ya watanzania) au wanapigania Taifa lao la wanamaslahi? Ni maslahi binafsi na ajenda za siri? Nasema tena na tena tuwakatae.