CCM yakoshwa na jinsi SMZ na SMT zinavyothamini wafanyakazi

0

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi kimepongeza hatua ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupandisha mishahara ya Wafanyakazi wa kima cha chini hadi kufikia Shilingi 500,000 kwa Mwezi.

Aidha, Wafanyakazi katika Sekta ya Umma na Binafsi, sasa wametakiwa kuongoza juhudi, bidii na nidhamu ya Kazi kama msingi unaokuza shime ya Maendeleo.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo alipozungumza na Wandishi wa habari katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Kisiwani Unguja.

Mbeto alisema, CCM imeziagiza Serikali zake kuhakikisha zinaendelea kutekeleza ahadi za kisera na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Vyama vya Wafanyakazi.

Alisema, sera za CCM ndizo zitaendelea kuzielekeza Serikali zake kushughulikia maslahi ya Wafanyakazi wa sekta ya Umma na binafsi ili haki na maslahi ya kila Mfanyakazi yakilindwa.

Alisema, CCM ndicho chenye wajibu wa awali wa kuzikumbusha Serikali, zitekeleze sera zake kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani yake ya Uchaguzi.

“Serikali ya Rais Dkt Samia na Rais Dkt. Huseein Mwinyi ni sikivu zinazoshughulika na changamoto za Wafanyakazi wa kima cha chini ili kuwapatia ustawi bora,” alisema Mbeto.

Alisema, CCM kinawataka Watendaji wote dhamana katika Wizara za Kazi na Ajira, SMZ na SMT, watimize wajibu walionao bila longolongo na urasimu,” alisema Mbeto.

Akizungumzia upande wa SMZ, Mbeto aliongeza kusema, SMZ imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha maslahi ya Wafanyakazi ikiwemo nyongeza ya mishahara, huduma ya Afya ili kuchochea utekelezaji bora wa Majukumu ya Wafanyakazi.

Aidha, SMZ chini ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi inatambua na kuthamini Kazi kubwa inayofanywa na Wafanyakazi ya kuleta Maendeleo, Kukuza Uchumi na Ustawi wa jamii katika Sekta mbalimbali.

“CCM inaridhishwa na juhudi zianzochukuliwa na SMZ na kuwaahidi Wafanyakazi maisha bora. Serikali iko katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kuongeza mshahara baada ya Bajeti ya SMZ mwaka 2025-2026,” alisema.

Hata hivyo, Katibu huyo Mwenezi alisema CCM kinaona fahari kwa Serikali zake zikifanya juhudi za kuhangaikia maslahi ya Wafanyakazi yatakayiboresha maisha yao.

Mbeto alisema, kama ilivyo kwa Ndovu hashindwi kuubeba mkonga wake, CCM hakitawahi hata mara moja kuchoka kushughulikia matatizo ya jamii iikiwemo Wafanyakazi .

”Tutashirikana na Viongozi wa jumuiya za Wafanyakazi na wadau wengine katika jamii. Nia ni kuinua kiwango cha maisha ya Wafanyakazi. Tungependa kuona maisha yao yakitononeka,” alieleza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here