. Yazoa wanachama zaidi ya 2,439
Mwandishi Wetu, Pemba
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeibomoa ngome ya ACT Wazalendo baada ya wanachama zaidi ya 2,439 kurudisha kadi za chama hicho kwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mauani, Kiwani, Kusini Pemba.
Katika mkutano huo ambao ilikuwa sehemu ya mapokezi ya Rais Dkt. Mwinyi ambaye Katika mkutano Maalum wa chama hicho, uliofanyika Dodoma 18 na 19 Januari mwaka huu, jina lake lilipitishwa kuwania tena Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mkutano mkuu huo CCM, ulipitisha jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika mkutano Maalum wa chama hicho, uliofanyika Dodoma 18 na 19 na kuidhinisha uteuzi wa Makamu Mwenyekiti (Bara), Steven Wassira.
Wanachama waliotangaza kukihama chama cha ACT Wazalendo ni wanachama wa kawaida na viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa na wilaya ambao walitumbukiza kadi zao katika fuko alilokuwa amelishika Rais Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi ikabidi asaidiwe kulibeba fuko hilo na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika mkutano huo ambao uliotanguliwa na maandamano makubwa toka Uwanja wa ndege hadi ofisi za CCM Mjini Pemba na baadae hadi viwanja hivyo vya Mauani.
Rais Dkt. Mwinyi alishukuru umati uliojitokeza na kuwataka kufanya hivyo pia siku ya kupiga kura ili kuhakikisha unapatikana ushindi ambao haujawahi kutoka.

Alisema, umati huo wa watu unaonyesha jinsi gani walivyo na mapenzi kwake na anawashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu waliopitisha jina lake na kuwataka wananchi na wanaCCM Pemba kumpa kura za kutosha ili kukamilisha miaka mingine mitano ili kuwaleta maendeleo zaidi.
Awali, akizungumza wakati wa mkutano huo, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Abdulla alisema, Dkt. Mwinyi ni mtu wa vitendo zaidi na sio maneno na ndio maana sasa yanashuhudiwa maendeleo ambayo hayakuwahi kufikiriwa.

Katibu Kamati ya Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema kuwa huo ni mwanzo tu na wale ambao walikuwa wakifikiria kungekuwa na maigizo walijidanganya.
“Kina Jussa ndio muone sasa kama ni maigizo” alisema Mbeto na kuongeza kuwa atahakikisha ACT Wazalendo ‘inafutika’ Pemba kwani wananchi wa Zanzibar wamechoshwa na ubabaishaji walichokuwa wanataka ni maendeleo na sasa wanayaona.