DAR ES SALAAM, mji unaokua kwa kasi na wenye mahitaji makubwa ya maji, hatimaye utaondokana na kero ya uhaba wa maji kufuatia utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema kuwa mradi huu utakuwa suluhisho la kudumu kwa jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wake.
Akitoa pongezi kwa waandishi wa habari kwa juhudi zao za kupaza sauti kuhusu changamoto za maji, Balile alisisitiza kuwa mchango wa vyombo vya habari umechangia pakubwa katika kuhakikisha serikali inachukua hatua.
Serikali, kupitia uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imeanza kutekeleza mradi huu mkubwa kwa uhakika na weledi.
Bwawa la Kidunda litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji, huku likitarajiwa kutiririsha lita bilioni 2 kwa siku katika kipindi cha kiangazi cha Septemba hadi Novemba.
Hili litasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Pwani, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo.
Mbali na uhifadhi wa maji, mradi huu pia unajumuisha ujenzi wa mtambo wa kuzalisha megawati 20 za umeme kwa saa, ambao utaunganishwa kwenye gridi ya taifa kupitia njia ya kusafirisha umeme ya 132kV kutoka Kidunda hadi Chalinze.
Hili ni ongezeko kubwa katika uzalishaji wa nishati, ambalo litaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini.
Miundombinu ya usafirishaji nayo imepewa kipaumbele, ambapo barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 75 kutoka Ngerengere hadi eneo la mradi imejengwa.
Hii itawezesha usafiri wa haraka wa vifaa na wafanyakazi, na baadaye kutoa fursa kwa wananchi wa maeneo jirani kutumia barabara hiyo kwa shughuli zao za kila siku.
Mradi huu wa kimkakati ulianza kutekelezwa Juni 18, 2023 baada ya serikali kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 335.8. Utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika Juni 17, 2026, hatua itakayohakikisha wakazi wa Dar es Salaam na Pwani wanafurahia huduma bora ya maji na nishati kwa miaka mingi ijayo.