Bilioni 1.7 kuboresha huduma za afya Sumbawanga

0

Na Jumbe Abdallah


HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imepokea jumla ya Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Saba Hamsini ( 1.75 Bilioni) kwa ajili ya kukamilisha majengo na ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali ya manispaa ya Sumbawanga na baaadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya.


Mkuu wa idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe wa manispaa ya Sumbawanga Dkt. Sebastian Siwale amesema, fedha hizo zitatumika kukamilisha jengo la utawala na wodi ya kujifungulia,ujenzi wa kituo cha afya kata ya Senga na Zahanati.


“Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea hizi fedha amabazo tutazitumia kwenye kuendeleza ujenzi wa hospitali yetu ya Manispaa, kumalizia ujenzi wa kituo cha afya na umaliziaji wa zahanati moja. Pia tunategemea hadi mwishoni mwa oktoba mwaka huu kukamilisha ujenzi wa zahanati mbili za Mponda na Kingombe.”


Dkt. Siwale ameongeza, katika fedha hizo, Shilingi Milioni 130 zitatumika katika ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya katika manispaa hiyo.


Kabla ya kupokea fedha hizi, Manispaa ya Sumbawanga ilipokea jumla ya Shilingi Milioni 900 mwaka jana mwishoni kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya manispaa ya Sumbawanga.


Miradi hiyo imekamilika na kuzinduliwa na mbio za mwenge Agosti 31, 2023. Pia, Manispaa ya Sumbawanga imetumia Shilingi Milioni 150 kujenga zahanati tatu za Fyengerezya, Kankwale na Nambogo ambazo zimeanza kufanya kazi ya kuhudumia wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here