Bandari ya Dar es Salaam yavutia Mataifa ya Ulaya, Asia na Afrika

0

Na Mwandishi Wetu

MABORESHO makubwa na uwekezaji unaoendelea kufanywa katika Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa kivutio kwa Mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya kuja kuangalia na kushuhudia utendaji kazi wake na uwezekano wa kuanza kufanya kazi nao.

Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Jemedari Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitatu, imeiboresha bandari ya Dar es Salaam kwa kuruhusu wawekezaji ambao ni DP World ambaye anasimamia gati namba 4 mpaka 7 pamoja na Adan International Ports Holding ambaye anasimamia gati namba 8 mpaka 11.

Kutokana na maboresho hayo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mapema mwezi Novemba Umoja wa Wafanyabiashara kutoka nchini Kongo katika miji ya Kalemie, Uvira, Bukavu na Goma walitembelea bandari ya Dar es Salaam na kujionea jinsi kazi zinavyofanyika na kuangalia maboresho yalipofikia.

Uongozi huo wa Wafanyabiashara ulipokelewa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Lufunyo Hussein ambaye aliwashukuru wafanyabiashara hao kwa kutembelea na kuendelea kutumia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Kigoma.

Lufunyo aliwahakikishia Usalama wa mizigo yao kwa kusema wamefunga kamera zaidi ya 400, ambazo zinafanya kazi usiku na mchana na muda wote wa masaa 24 pamoja na wataalamu wanaozisimamia.

Hata hivyo, Serikali za nchi hizi Mwezi Juni mwaka huu zimesaini mkataba wa uendelezaji wa Bandari kavu za Kwala na Katosho za nchini Tanzania, na bandari kavu za Kasambondo na Kalemie za huko nchini Kongo kwani takwimu zinaonyesha nchi ya Kongo inaongoza kwa kupitisha kiasi kikubwa cha shehena kupitia bandari ya Dar es Salaam ambapo katika mwaka 2022/2023 tani Milioni 3.5 za shehena zilipitishwa.

Taarifa iliyotolewa na TPA imesema soko kubwa la bandari ya Dar es Salaam lipo nchini Kongo kwani hupitisha bidhaa mbalimbali hasa za madini na wao hupokea bidhaa wa kadha wa kadha za viwandani kutoka katika nchi za Asia na Ulaya ambazo zinapitia bandari ya Dar es Salaam.

Mapema mwezi wa tisa mwaka huu, uongozi wa TPA ulikutana na Uongozi wa Shirika la meli la COSCO kutoka nchini China, ambapo walijadiliana masuala mbalimbali pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya COSCO na TPA.

Uongozi wa COSCO uliuhakikishia uongozi wa TPA kuleta meli na wateja ili waweze kutumia bandari ya Dar es Salaam kwani wamekiri kuridhishwa na utendaji kazi wake.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) nayo haikuwa nyuma katika kutembelea bandari ya Tanga, na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa katika miradi mbalimbali na maboresho ya bandari yenye lengo la kuongeza ufanisi na kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi.

Pia, TPA ilitembelewa na Balozi wa Uholanzi nchini Wiebe De Boer pamoja na ujumbe wake walitembelea bandari ya Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara.

“Nimefurahi kuona meli za bidhaa mbalimbali zinahudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam na makasha yanashushwa katika muda mfupi na kwa haraka zaidi” alisema De Boer.

Licha ya TPA kutembelewa na Serikali za nchi za nje pia ilitembelewa na Kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen ya nchini Ujerumani imeonesha nia ya kuitumia bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha magari na vipuri kwa wateja wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Walitoa ahadi hiyo Septemba mwaka huu mara baada ya kutembelea bandari hiyo na kuikagua ndipo wakaridhishwa na kusema inakidhi vigezo vya kimataifa na kuahidi kuitumia kwa ajili ya biashara hiyo.

Akiongea baada ya kutembelea eneo la kuhifadhia magari yanayowasili bandarini hapo kutoka nje ya nchi, Rais wa kampuni hiyo Martina Biene kwa nchi za Afrika ambaye pia ni Rais wa Chama cha Watengeneza magari Afrika (AAAM) amesema kuwa wameamua kuitembelea bandari ya Dar es Salaam na kuangalia namna inavyofanya kazi na uwekezaji uliofanyika ili kufanya kazi pamoja.

“Kupitia maboresho haya, Bandari ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa sana katika ukuaji wa nchi katika bara la Afrika kwa sababu imekuwa ni kitovu cha biashara katika nchi nyingi katika bara hili,” alisema Biene.

Biene anasema, wakiwa ni wazalishaji wa magari na vipuri katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo bara la Afrika, wanaiona Bandari, hii ni kama kichocheo kikubwa cha biashara barani Afrika.

Katika mnyororo wa biashara ni lazima na inashauriwa sana kufanya utafiti katika njia zote ambazo biashara hiyo itapita ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza au kuwa kikwazo cha biashara husika.

Inasemekana watu wengi au makampuni mengi wanashindwa kuendelea au kusimamia biashara na hupelekea kuzifunga mara tu wanapoanza biashara hizo na sababu kubwa inayopelekea kufunga biashara zao mapema ni kwa sababu hawakufanya utafiti wa kutosha kuhusu biashara husika.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikafanya utafiti wa kutosha na kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili bandari zetu ziwe na tija zaidi na ziweze kushindana na bandari za majirani zetu.

Ndipo wakaja na mapendekezo kadhaa ambayo miongoni mwa hayo ni kukubali maombi ya uwekezaji katika bandari zetu hususani bandari ya Dar es Salaam, kuongeza kina cha maji katika bandari hiyo na kuongeza vifaa vya kushushia mizigo na kupakia, kuongeza kamera za ulinzi na kufungua ofisi za Bandari katika nchi za Malawi na Zimbabwe ikiwa na lengo la kuvutia zaidi wafanyabiashara waje watumie bandari ya Dar es Salaam.

Ili kuongeza ushindani wa kibiashara katika soko la Bandari za Tanzania, Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu yake yote kwa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, na Mbambabay katika Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma na bandari za mkoani Kigoma.

Uimarishaji wa Bandari ya Tanga utasaidia katika kusafirisha mizigo yote ya kanda ya Kaskazini, na hii ni kwa mikoa ya Tanga, Arusha na Manyara, lakini pia itaweza kuhudumia mikoa ya Mara na Mwanza.

Bidhaa zote za kutoka na kuingia ughaibuni zinaweza kufika kwenye mikoa hiyo bila ya kuchelesha.

Kukamilika kwa maboresho ya bandari ya Mtwara itasaidia sana kwa soko la Kusini mwa Tanzania na hii ni kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, lakini pia kupeleka huduma mpaka kwenye mikoa ya Njombe Mbeya na Songwe.

Aidha, bandari hiyo itasaidia kusafirisha shehena za mazao kutoka kwenye mikoa hiyo na kwenda nchi za ughaibuni.


Faida ya uwekezaji huu inaenda kwa wadau mbalimbali kama vile wakulima wa mazao ya korosho, mtama, mbaazi na ufuta, lakini pia wafanyabiashara wa mazao hayo wataneemeka kwa sababu watapata masoko mapya ya mazao yao na Serikali yenyewe kwani wanapata mapato kupitia kodi (import duties).

Mazao makubwa ya biashara yanayozalishwa kwenye mikoa hiyo ni pamoja na korosho, ufuta na mbaazi, ambayo kwa kiasi kikubwa huuzwa nchi za Uarabuni, hivyo bandari hiyo itakuwa na tija sana kwa wakulima, wafanyabiashara pamoja na Serikali kwa ujumla.

Uboreshwaji wa hizi bandari utaendelea kuifungua nchi yetu Kitaifa na Kimataifa kwa kiasi kikubwa kwani bandari ya ziwa Nyasa itatuunganisha vizuri sana na nchi ya Malawi, itawezesha wafanyaiashara wa kitanzania kwenda kuuza bidhaa zao Malawi pia kuleta bidhaa kutoka Malawi kwa ajili ya soko la Tanzania.

Vivyo hivyo, bandari za ziwa Tanganyika zitafungua nchi hasa kwa kuuza mazao ya Tanzania kama vile mahindi, mpunga na maharage kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Rwana na Burundi.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Plasduce Mbossa ilisema kuwa asilimia 95 ya shehena zote zinazoingia nchini hupitia kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumzia kuhusu bandari ya Dar es Salaam amesema, mpaka sasa TPA inaendelea na ujenzi wa magati mapya kumi na wapo kwenye mpango wa kujenga magati mengine mapya mawili hivyo kufanya kuwa na magati kumi na mawili katika bandari ya Dar es Salaam, kwa kiasi kikubwa itachochea uchumi wa nchi.

“Kuongezeka kwa gati hizo kutachochea ongezeko la wateja wa ndani ya nchi sambamba na nchi jirani zinazotutuzunguka ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Malawi,” anasema Mbossa.

Katika kukuza mashirikiano na nchi za jirani na kuendelea kuzishawishi ziweze kuendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam, Mbosa anasema tayari wamekwishafungua Ofisi za TPA katika nchi za Malawi na Zambia, kwa lengo la kuwafikia wateja moja kwa moja, nchi hizo hutegemea bandari ya Dar es Salaam kwa kuingiza mizigo yao kutoka nchi za nje.

“Ujenzi wa haya magati pamoja na ufunguzi wa ofisi zetu katika nchi tajwa utasaidia sana kupunguza foleni kwa wateja lakini pia kuongeza idadi ya wateja’’ aliongeza Mbossa.

Hapo awali meli ikishafika katika eneo la Bandari ya Dar es Salaam ilikua inachukua siku 30 mpaka kushusha shehena hiyo, lakini kwa sasa inachukua siku nne mpaka tano tu.

Pamoja na maboresho hayo Mbossa anasema kwa sasa bandari ya Dar es Salaam hupakua makontena laki moja kwa mwezi kutoka makontena elfu sabini hapo awali, na ongezeko la ujenzi wa hizo gati utapelekea kushusha idadi kubwa zaidi ya makontena kwa mwezi.

Licha ya maboresho yanayofanywa na TPA, Mbossa anasema kuwa wanaendelea kuboresho mfumo wa malipo wa kidigiti ambao utamuwezesha mteja kufanya malipo popote pale alipo.

Kwa upande wa kuchangia pato la Taifa Mbossa amesema TPA inachangia zaidi ya asilimia 7.3 kwa mwaka, lakini lengo ni kuhakikisha sektra hiyo inachangia asilimia 15 ya pato la Taifa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here