Auba athibitisha Arteta anajua, Arsenal wakiilaza Chelsea 1-0

0

KLABU ya soka ya Arsenal, imerejea tena kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya soka nchini Uingereza, baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea, katika pambano lililopigwa dimba la Stanford Bridge. 

Bao pekee katika mchezo huo lilipatikana kunako dakika ya 63 ya mchezo, baada ya beki wa kimataifa wa Brazil, Gabriel Magalhães kuusindikiza wavuni mpira wa kona uliochongwa na Bukayo Saka na Arsenal wakafanikiwa kulinda bao hilo hadi mwisho wa mchezo. 

Pengine kwa mashabiki wa Arsenal, kushinda inaelekea kuwa jambo la kawaida kwao, na ndio sababu gumzo kwenye mechi hiyo halikuwa juu ya ushindi huo unaowafanya kufikisha pointi 34 baada ya mechi 13, pointi mbili mbele ya bingwa mtetezi Manchester City mwenye pointi 32 baada ya kucheza idadi hiyo hiyo ya mechi. Gumzo kuu limekuwa Piere Emerick Aubameyang. 

Miezi 12 iliyopita, Mchezaji huyo wa kimataifa wa Gabon, maarufu kama Auba, alikuwa nahodha wa Arsenal, katika kipindi ambacho klabu ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha kujiimarisha na akiwa mmoja wa wachezaji wakongwe katika klabu, ambaye klabu ilivunja rekodi zake kwa kumsajili kwa paundi za Uingereza milioni 60, alitarajiwa kuwa jiwe la msingi katika kuitengeneza Arsenal iliyokuwa imepoteza uelekeo.

Hata hivyo, Auba akaanza kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kuripoti kambini kila alipokuwa akipewa ruhusa kushughulikia masuala yake ya kifamilia. Mikel Arteta ambaye alikuwa hana muda mrefu tangu achukue timu, alivumilia hali hiyo lakini alipokinaishwa nayo, akachukua maamuzi magumu kwa maslahi ya klabu. 

Kwanza alimvua unahodha, kabla ya kuanza kumsugulisha benchi, kisha kuamuru afanye mazoezi na Kikosi B ili awe mbali kabisa na kikosi cha kwanza ambacho kilikuwa kinaonyesha uelekeo mzuri kwenye ligi, licha ya uchanga wake. 

Arteta alifanya hivi akiamini bila yeye kama mwalimu kuchukua hatua, tabia hiyo itaambukizwa kwa wachezaji makinda wanaoibukia na haitakuwa na manufaa kwa timu. Lakini uamuzi wake huo haukupokelewa vyema na mashabiki wengi wa Arsenal, ambao walikuwa wanaamini kuwa timu yao bila Auba, ilikuwa si chochote, si lolote.

Lakini kocha hiyo Mhispania, alisimama kwenye msimamo wake na kilichofuata baada ya hapo ni kama historia inavyoonyesha.

Arsenal na Auba wakakubaliana kuvunja mkataba baina yao na mchezaji kutimkia zake Barcelona bure kabisa. Hata hivyo, huko nako akadumi kwa miezi takrban sita tu mwanzoni mwa msimu huu Chelsea wakambeba wakiamini kuwa ulikuwa msumari wa mwisho kukamilisha paa la nyumba yao. 

Mechi ya leo ikawa ya Arsenal kusaka pointi tatu ambazo walizipata na kwa upande wa pili ikawa ya Auba kutaka kuudhihirishia umma kuwa Arteta alikosea sana kumuacha, jambo ambalo liliishia kwa Arteta kuonekana mshindi pia. 

Kwa zaidi ya dakika 60 alizokuwa dimbani, Auba alifanikiwa kugusa mpira mara nane tu, nne kati ya hizo ikiwa katika dakika 45 za kipindi cha kwanza na hata alipokiwa akifanyiwa mabadiliko huku timu yake ikiwa iko nyuma kwa bao 1-0, mashabiki wa Arsenal wakasikila wakiimba “amerejea na amerejeshwa benchi”.

Baadhi ya mashabiki walioandika mitandaoni baada ya pambano hilo wamesema wanamuomba msamaha Arteta kwani anajua analolifanya. 

“Niwe muungwana, nilikuwa mmoja wa waliomponda sana Arteta kuhusu Auba, lakini sasa naona sio tu kuwa alikuwa analeta kasumba mbaya kwa wachezaji, bali pia muda wake wa kutumika kama mchezaji mkubwa na tegemeo, ulishaanza kuelekea ukingoni…nisamehe Arteta” aliandika shabiki mmoja kwenye ukurasa wake wa Instagram. 

Naam, mechi baina ya Arsenal na Chelsea imemalizika kwa wekundu hao wa London Kaskazini kuibuka vinara na mechi baina ya Auba na Arteta pia imeibuka kwa mwalimu wa Arsenal kushinda. Je, nini kinafuatia? Arsenal ni washindani rasmi wa ubingwa msimu huu? 

Maswali yanaweza kuwa mengi sana, ila kwa sasa mashabiki wa Arsenal wala hawajali hilo. Wanafurahia kile kinafanywa na timu yao, wakifurahia pia kuzidi kuimarika kwa uhusiano baina ya timu na mashabiki.

Mengine wenyewe wanasema “tunachopaswa ni kushinda pambano linalokuwa mbele yetu, kisha mwisho wa ligi namba zitaongea”

Timu 10 za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Soka nchini Uingereza baada ya mechi za wikiendi hii


Imeandaliwa na Rama Msangi+255 767 412176 (Whatsapp tu)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here