Na A/INSP Frank Lukwaro – Jeshi la Polisi
MAOFISA, Wakaguzi, Askari na watumishi raia ndani ya Jeshi la Polisi wametakiwa kuhakikisha wanajiunga na vyama vya ushirika waweze kuboresha ustawi wao kiuchumi ikiwemo kurahisisha utendaji na kuongeza ufanisi katika kazi, hivyo kuwaepusha kushawishika kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa pindi wanapokabiliwa na mahitaji ya pesa kwa ajili ya maendeleo yao.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha Ushirika cha kuweka na kukopa cha Jeshi la Polisi (URA SACCOS) uliofanyika jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Sagini alisema, matumizi mazuri ya vyama vya ushirika yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua vipato vya watumishi kwa kuwa vimekuwa vikitoza riba nafuu katika mikopo na huduma zake kutokuwa na masharti magumu kulinganisha taasisi zingine za kifedha.
“Angalieni pia fursa za kuwekeza katika miradi ambayo itaongeza faida kwa kuwa fursa hizo zipo nyingi na hapa mtaweza kugawana na wanachama wenu hivyo kuendelea kuwa mfano wa chama imara kwa vingine,” alisema Sagini.
Aidha, alikipongeza chama cha URA SACCOS kwa kuendelea kupata tuzo za chama bora cha Ushirika wa Akiba na Mikopo kila mwaka ikiwemo kupata tuzo ya hati safi kutoka kwa mkaguzi wan je, Pamoja na kupata tuzo ya hati safi bora kati ya vyama 1849 vilivyokaguliwa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi la vyama vya Ushirika Tanzania mwaka 2021.
Kwa Upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa kifedha, CPA Josephat Kisamalala alisema Chama hicho cha Jeshi la Polisi ni mfano wa kuigwa kutokana na kuzingatia taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika Pamoja na kukua kwa kasi ukilinganisha na vyama vingine hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba alisema, mpaka kufikia Septemba 30, 2022 jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi 394,567,811,785 ilitolewa ambapo asilimia 75 ya mikopo hiyo wanachama walitumia katika ujenzi binafsi wa makazi.